Amnesty yaikosoa Nigeria kwa kuwakandamiza Waislamu wakiitetea Gaza
Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Nigeria, Isa Sunusi, amelaani vikali ukandamizaji mkali wa vyombo vya serikali dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, wakati wa maandamano ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kusema kuwa takriban wanachama 83 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria bado wako rumande bila kufunguliwa mashtaka, licha ya kupata majeraha ya risasi na makovu mengineo wakishiriki maandamano ya amani.
Katika mahojiano maalum na shirika la habari la Iran Press mjini Abuja, Sanusi amesema: "Kinachotokea Palestina ni doa kwa ubinadamu, mauaji ya halaiki yanaendelea. Watu wanapaswa kuandamana bila woga au kunyanyaswa. Kwa bahati mbaya, serikali ya Nigeria inawalenga wafuasi wa Shia kwa mauaji, utekaji nyara na kuwapoteza.
Ameeleza bayana kuwa, serikali ya Nigeria imekuwa ikijibu maandamano kwa nia ya kuua, na wala sio kudumisha utulivu, na kwamba vitendo hivyo vinakinzana na haki za kikatiba za uhuru wa kuabudu, dini na kukusanyika. Sanusi amesisitiza kuwa, ukandamizaji huo ni ukiukaji mkubwa na wazi wa haki za binadamu.
Afisa huyo mwandamizi wa Amnesty International nchini Nigeria amebainisha kuwa, "Tunatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wanachama wote (wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria) waliowekwa kizuizini, haki kwa wale waliouawa, na fidia kwa familia zao. Maandamano si jinai, yanapaswa kuwa ya amani. Maandamano ya Nigeria yanapasa kuwa ya amani kama ilivyo duniani kote."
Wanachama wasiopungua 83 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wakiwemo wanawake, watoto, na hata mtoto mchanga wa mwezi mmoja na mama yake, wanashikiliwa katika magereza ya Kuje na Suleja bila kufungulia mashitaka, baadhi yao wakiwa na majeraha ya risasi ambayo hayajatibiwa, licha ya malalamiko ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, makumi ya watu walipoteza maisha nchini Nigeria huku vikosi vya usalama vikikabiliana kwa mabavu na maandamano ya amani ya Siku ya Quds ya mwaka huu 2025 huko Abuja na Kaduna.