Wabunge chipukizi waapa kukomboa Kenya, watadhamini mgombea urais 2027
Kundi la Kenya Moja, linaoshirikisha wabunge chipukizi, limeahidi kudhamini mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu ujao na kuahidi kufanya “ukombozi wa tatu nchini humo”.
Wanachama wa kundi hilo, waliochaguliwa kwa tiketi za vyama vya ODM, UDA, Ford Kenya na DAP-K, wanasema wanataka kufanya mabadiliko ya kweli yanayoakisi matarajio ya kizazi cha kisasa cha Wakenya maarufu kama Gen-Z.
“Sisi kama viongozi wa kizazi cha sasa, tuko tayari kuchukua uongozi wa taifa hili mwaka wa 2027 kwa kudhamini mgombeaji wa urais", wamesema viongozi wa kundi hilo.
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ambaye ni mmoja wa vinara wa vuguvugu hilo amesema: “Kenya Moja si mrengo wa tatu kama wengine wanavyodai; huu ndio mrengo mkuu kwa sababu Wakenya wa umri wa chini ndio wengi zaidi nchini.”
Mbio za kuwania urais wa Kenya mwaka wa 2027 zimeanza kushika kasi, huku kikundi cha viongozi chipukizi kikijitokeza na kuanza kuvutia hisia za Wakenya, hususan tabaka la vijana.
Kwa mujibu wa viongozi hao, Kenya Moja inalenga kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuondoa hali wanayoiita 'uongozi wa kizazi kilichoshindwa kutimiza matarajio ya wananchi kwa miaka mingi'.