Marufuku ya kutotoka nje yawekwa maeneo yenye ghasia za kikabila Kenya
Serikali ya Kenya imetangaza kuweka marufuku ya kutotoka nje katika maeneo yenye ghasia za kikabila katika nchi hiyo ya Afrika Mashaariki.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mamlaka husika nchini Kenya imetangaza kuwa, imeweka marufuku ya kutotoka nje kwa siku saba kuanzia jioni hadi alfajiri katika baadhi ya sehemu za kaunti ya Nakuru baada ya kuzuka ghasia za kikabila.
Takriban mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa huku nyumba takriban 12 zikichomwa moto kufuatia mapigano ya kikabila yaliyoibuka huko Tipis na maeneo ya Mwisho wa Lami.
Vurugu hizo, ambazo ziliibuka siku ya Jumamosi katika mpaka wa Nakuru -Narok, zilisababisha familia kadhaa kuhama makazi yao baada ya washambuliaji kuchoma moto nyumba na kuharibu mali.
Kufikia siku ya Jumapili 30/08/2025, hali ya wasiwasi bado ilikuwa juu wakaazi walipofunga sehemu za Barabara ya Nakuru -Narok huko Mwisho Wa Lami, wakipinga mauaji hayo na kudai serikali iingilie kati.
Kufuatia ghasia hizo, serikali ya Kenya imetangaza kuwa, imechukua hatua ya kupeleka maafisa wa usalama katika eneo hilo kwa ajili ya kkudhibiti hali ya mambo na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.