Misri kutuma vikosi vya kulinda amani Somalia huku Ethiopia ikionyesha wasiwasi
Misri inapanga kutuma kikosi cha kulinda amani nchini Somalia chini ya Mpango wa Msaada wa Umoja wa Afrika kwa Somalia (AUSSOM). Ingawa Ethiopia haijatoa kauli ya wazi, lakini huko nyuma ilibainisha kutoafiki ushiriki wa wanajeshi wa Misri katika kikosi hicho cha Umoja wa Afrika.
Hatua hiyo haijapokelewa vizuri na viongozi wa Ethiopia, ambao wameonya kuwa uwepo wa wanajeshi wa Ethiopia na Misri ndani ya AUSSOM unaweza kuchochea mzozo baina yao.
Misri, ambayo imechukua msimamo mkali zaidi katika mvutano wake na Ethiopia kuhusu bwawa ambalo Ethiopia inajenga katika Mto Nile, ilianza kupeleka vifaa vya kijeshi na msaada kwa Somalia mwaka jana.
Mnamo Jumatatu, ujumbe wa wanajeshi 16 kutoka Jeshi la Misri uliwasili Mogadishu kwa ajili ya uchunguzi wa awali kabla ya mpango wa Cairo wa kupeleka vikosi.
Balozi wa Ethiopia nchini Somalia, Suleiman Dedefo, aliviambia vyombo vya habari vya Kisomali hivi karibuni kuwa Addis Ababa inaamini kuwa jukumu la Misri si tishio la moja kwa moja, akiongeza, “almradi wasijaribu kukabiliana na vikosi vyetu.”
Suleiman alinukuliwa pia akisema, “Kama Wamisri wana faida yoyote, basi iwe katika nchi jirani kama Palestina, Libya au Sudan.”
Kauli yake ilikuja siku moja baada ya wanajeshi wa Misri kukamilisha mafunzo yao ya awali kwa ajili ya kujiunga na AUSSOM.
Ujumbe wa Misri uliowasili Mogadishu, ukiongozwa na Meja Jenerali Islam Radwan, ulipokelewa na maafisa kutoka AUSSOM na Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNAF).
Baadaye walifanya mazungumzo na uongozi wa AUSSOM, wakiwemo Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (SRCC) na Mkuu wa Ujumbe, Balozi El Hadji Ibrahima Diene, na kuhudhuria kikao cha usalama katika Makao Makuu ya Vikosi vya AUSSOM jijini Mogadishu.