Njaa yaongezeka nchini Nigeria sambamba na kupungua usambazaji wa chakula
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130422-njaa_yaongezeka_nchini_nigeria_sambamba_na_kupungua_usambazaji_wa_chakula
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema watu milioni 31 wanakabiliwa na uhaba wa chakula nchini Nigeria, hasa kaskazini mashariki, ambako watu milioni 2.3 wamelazimika kuacha makazi na mashamba yao katika kipindi cha miaka 15 ya vita.
(last modified 2025-09-04T22:53:15+00:00 )
Sep 04, 2025 22:53 UTC
  • Njaa yaongezeka nchini Nigeria sambamba na kupungua usambazaji wa chakula

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema watu milioni 31 wanakabiliwa na uhaba wa chakula nchini Nigeria, hasa kaskazini mashariki, ambako watu milioni 2.3 wamelazimika kuacha makazi na mashamba yao katika kipindi cha miaka 15 ya vita.

Ripoti zinasema, familia zilizopoteza makazi kutokana na mzozo kaskazini mashariki mwa Nigeria zinajipata katika hali ya kusikitisha kutokana na kufungwa vituo vya kugawa chakula kutokana na kusita ufadhili wa misaada kutoka za Magharibi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa "watu milioni 31 wanakabiliwa zaidi na uhaba wa chakula nchini humo, kuliko nchi nyingine yoyote, na kwamba hali mbaya zaidi inashuhudiwa kaskazini mashariki, ambapo watu milioni 2.3 wamelazimika kuacha nyumba na mashamba yao katika kipindi cha miaka 15 ya vita kati ya waasi na jeshi la Nigeria."

Kwa mujibu wa Reuters, matokeo ya nyandani nchini Nigeria yanaonekana kuwa mabaya. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani lilifunga vituo 150 vya kugawa chakula kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wakati wa msimu wa kiangazi, ambao unaanza Juni hadi Novemba, huku mashirika mengine ya misaada yakifunga milango yao kabisa.

Chi Lel, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani nchini Nigeria amesema: "Hii ina maana kwamba mamia ya maelfu ya watoto wamekosa kupata matibabu muhimu, na idadi ya watoto wanaohitaji kulazwa hospitalini imeongezeka kwa kiasi kikubwa."

Wiki iliyopita, shirika la Save the Children lilikadiria kuwa watoto milioni 3.5 kote nchini Nigeria wanahitaji matibabu kutokana na utapiamlo mkali.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limeripoti kwamba "mgogoro unaowakabili watoto nchini Nigeria haujawahi kutokea. Watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali wana uwezekano mkubwa wa kufa kutokana na magonjwa ya kawaida kuliko watoto walio na lishe bora."