Misri: Ni 'upuuzi' kuelezea kuhama kwa Wapalestina ni kwa hiari
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri, Badr Abdelatty, amesema kuwa, kuelezea uhamisho wa Wapalestina kama ni wa hiari ni “upuuzi.”
Awali, Israel iliwataka wakazi wa Jiji la Gaza kuhamia kusini, huku vikosi vyake vikisonga zaidi ndani ya eneo kubwa zaidi la mijini la Ukanda huo.
Vikosi vya utawala wa kizayuni wa Israel vimekuwa vikitekeleza mashambulizi katika vitongoji vya jiji la kaskazini kwa wiki kadhaa, baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuagiza jeshi kuchukua eneo hilo.
Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Misri amesisitiza kuwa, huwezi kuuelezea uhamaji huo kuwa ni wa hiari hata kidogo.
Kabla yah apo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilikuwa imelaani matamshi ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na kusisitiza kuwa Misri haitakuwa lango la kupitishia wananchi wa Palestina wanaohamishwa kwa nguvu katika ardhi yao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza hayo kupitia taarifa na kutangaza kuwa inapinga vikali jaribio lolote na linalofanywa kwa anuani yoyote, la kuwahamisha Wapalestina katika ardhi yao.
Kadhalika, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa wito wa kukabiliana na hali ya machafuko iliyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika eneo na kutahadharisha juu ya madhara yake kwa usalama na uthabiti wa eneo hili.
Matamshi ya Netanyahu ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza ikiwemo kupitia kivuko cha Rafah ambacho ni mpaka wa pamoja wa ukanda huo na Misri yamelaaniwa vikali na serikali za Misri, Qatar na Saudi Arabia.