Boko Haram yaua zaidi ya watu 60 kaskazini mashariki mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130508-boko_haram_yaua_zaidi_ya_watu_60_kaskazini_mashariki_mwa_nigeria
Kundi la wapiganaji wanaoaminikka kuwa wa Boko Haram limewaua zaidi ya watu 60 katika shambulio la usiku kwenye jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2025-09-07T03:07:11+00:00 )
Sep 07, 2025 03:07 UTC
  • Boko Haram yaua zaidi ya watu 60 kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi la wapiganaji wanaoaminikka kuwa wa Boko Haram limewaua zaidi ya watu 60 katika shambulio la usiku kwenye jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Chanzo cha usalama kimesema shambulio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi na kulenga kijiji cha Darul Jama, ambacho kina kambi ya kijeshi na nyumba za watu waliopewa makazi mapya baada ya kambi za wakimbizi wa ndani kufungwa. Chanzo hicho kimesema wanajeshi watano ni miongoni mwa waliouawa.

Wakazi wa eneo hilo wanasema, makumi ya washambuliaji walivamia kwa pikipiki mwendo wa saa mbili na nusu usiku na kuanza kufyatua risasi ovyo na kuchoma nyumba.

"Waliingia kwa makelele na kumpiga risasi kila mtu waliyemwona. Tuliporejea alfajiri, kulikuwa na miili kila mahali," amesema manusura, Malam Bukar.

Duru za usalama zimedokeza kuwa shambulio hilo liliongozwa na kiongozi mashuhuri wa Boko Haram, Ali Ngoldi, ambaye anajulikana kuwa ndiye anayedhibiti eneo hilo.

Maeneo ya katikati mwa Nigeria pia yanashuhudia mashambulizi kama hayo, na matukio hayo yameongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya usalama kudorora kutokana na harakati za makundi ya "kigaidi".

Kiongozi wa kitamaduni wa Darul Jama, ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba miili 70 ilikuwa imepatikana hadi asubuhi ya jana Jumamosi na kwamba raia zaidi walikuwa bado hawajulikani walipo katika msitu unaozunguka eneo hilo.