WHO: Njaa imeathiri baadhi ya maeneo ya Sudan
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunuani Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba "Sudan inakabiliwa na mgogoro wa uhaba wa chakula na njaa katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo," akieleza kuwa hali ni mbaya haswa katika eneo la Darfur Kaskazini, ambako mji wa El Fasher unazingirwa kwa zaidi ya siku 500.
Ghebreyesus ametoa wito wa kuwasilishwa haraka, kwa salama, na bila vikwazo misaada ya kibinadamu huko El Fasher ili kukidhi mahitaji ya afya yanayoongezeka na kuokoa maisha ya watu.
Haya yanajiri huku mapigano yakiendelea huko El Fasher kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan (kundi huru) ulitangaza Jumanne iliyopita kwamba raia 18 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa kutokana na mizinga ya risasi za wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka.
Siku chache zilizopita pia, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) nchini Sudan ilisema katika ujumbe uliowekwa kwenye jukwaa la X kwamba Sudan inakabiliwa na janga kubwa zaidi la uhaba wa chakula duniani.
Tangu katikati ya mwezi wa Aprili 2023, jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vimekuwa katika vita na mapigano ya ndani ambayo yameua zaidi ya watu 20,000 na kulazimisha wengine karibu milioni 15 kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.