DRC: Maelfu ya wanafunzi wa Kivu washindwa kurudi shule kutokana na mapigano
Maelfu ya wanafunzi wa Kivu Kusini na Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameshindwa kurudi shule kutokana na mapigano yanayoendelea katika majimbo hayo.
Mwaka wa shule, uliopangwa awali kuanza siku ya Jumatatu, Septemba 1, haukuanza tena katika shule kadhaa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya kundi la AFC/M23 na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na Wazalendo.
Hali hiyo inahatarisha mustakabali wa maelfu ya watoto, licha ya kujitolea kwa usitishaji vita kati ya pande hizo mbili ambazo ziko katika mazungumzo mjini Doha.
Katika mkoa wa Kivu Kaskazini, shule zilizoathiriwa ziko kwenye mpaka kati ya maeneo ya Walikale na Masisi. Katika maeneo hayo, madarasa hayakufunguliwa. Kutokana na hali hiyo ya ukosefu wa usalama, Kaurwa Hilaire, Mkuu wa Shule ya Msingi ya Showa iliyopo Masisi, anaeleza: "Mwaka wa masomo huko Showa, hatujui ni lini utaanza." Hadi 85% ya watu wametoroka makazi yao huko Masisi; hatutathubutu kufungua milango huko maana bado kuna ukosefu wa usalama.
Huko Kivu Kusini, maelfu ya wanafunzi pia wameshindwa kurejea shuleni katika eneo la Itombwe huko Mwenga. Hii pia ni kutokana na mapigano ya hivi karibuni kati ya waasi na jeshi linaloungwa mkono na Wazalendo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, makundi yenye silaha pamoja na vyombo vya dola katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamehusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.