Mamia waandamana Uvira, Congo DR, wanataka Jenerali Gasita aondolewe madarakani
Mamia ya wakazi wa Uvira, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waliandamana jana Jumatatu katika mitaa ya mji huo dhidi ya serikali wakiitikia wito wa mashirika ya kiraia.
Wananchi hao wanapinga uteuzi wa hivi majuzi wa Jenerali Olivier Gasita Mukunda kuwa naibu kamanda wa eneo la 33 la Jeshi la Kikosi cha Wanajeshi wa DRC (FARDC).
Waandamanaji wanataka Gasita aondolewe madarakani, wakimtuhumu kuwa alishirikiana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakati wa kutekwa mji wa Bukavu Februari mwaka jana.
"Tumeletewa afisa ambaye hatukubaliani naye, Jenerali Olivier Gasita. Ana rekodi mbaya sana huko Bukavu,"amesema mwndamanaji Dunia Prince.
Mapenzi Manyebwa, rais wa Harambee ya Jumuiya ya Kiraia ya Uvira, anahofia kwamba uteuzi wa Gasita ni ishara kwamba mamlaka ziko tayari "kukabidhi mji kwa waasi."
Polisi na jeshi walisimamia maandamano hayo, ambayo yaliendelea kwa amani hadi risasi za tahadhari zilipofyatuliwa wakati wa kutawanywa kwa maandamano hayo, na kusababisha hofu.
Mashirika ya kiraia yanaripoti vifo vya watu wasiopungua vinne na majeruhi kadhaa, idadi ambayo bado haijathibitishwa na serikali za mitaa.