Ethiopia yazindua bwawa kubwa zaidi la umeme barani Afrika, Misri yapinga mradi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130638-ethiopia_yazindua_bwawa_kubwa_zaidi_la_umeme_barani_afrika_misri_yapinga_mradi
Ethiopia imezindua rasmi Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), mradi mkubwa zaidi wa umeme wa maji barani Afrika, huku mvutano ukiongezeka na mataifa ya chini ya Mto Nile ambayo ni Misri na Sudan.
(last modified 2025-09-10T07:27:14+00:00 )
Sep 10, 2025 07:27 UTC
  • Ethiopia yazindua bwawa kubwa zaidi la umeme barani Afrika, Misri yapinga mradi

Ethiopia imezindua rasmi Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), mradi mkubwa zaidi wa umeme wa maji barani Afrika, huku mvutano ukiongezeka na mataifa ya chini ya Mto Nile ambayo ni Misri na Sudan.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed alifungua rasmi mradi huo wa dola bilioni 5 akiwa ameandamana na viongozi wa Afrika, akitangaza kuwa bwawa hilo litaangazia kanda nzima kwa nishati, huku akiwahakikishia majirani kuwa lengo lake si kuwatendea mabaya ndugu zake.

Abiy amesema: “Bwawa la Renaissance si tishio, bali ni fursa ya pamoja; nishati na maendeleo yatakayozalishwa ni kuinua si Ethiopia pekee, bali eneo zima.”

Bwawa hilo, lenye urefu wa mita 170 na likijivuta takriban kilomita 2 juu ya Mto Nile wa Bluu, lina uwezo wa kuzalisha megawati 5,150, idadi inayozidi mara mbili uzalishaji wa umeme wa Ethiopia kwa sasa.

Hifadhi ya maji ya bwawa hilo ina ujazo wa mita bilioni 74 za maji, jambo linalozua hofu nchini Misri ambako Mto Nile unatoa asilimia 97 ya mahitaji ya maji kwa watu wake milioni 100.

Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, amekuwa akilitaja bwawa hilo kubwa la  Ethiopia mara kwa mara kama tishio la kuwepo kwa taifa lake, akiahidi kulinda haki za maji za Wamisri.

Licha ya Ethiopia kutoa hakikisho kuwa mradi huo hauna madhara, Misri na Sudan zinataka makubaliano ya kisheria kuhusu uendeshaji wa bwawa hilo na usimamizi wa vipindi vya ukame.

Tafiti huru zinaonyesha kuwa hakuna madhara makubwa yaliyotokea hadi sasa, jambo linaloelezwa kuwa ni matokeo ya kujaza hifadhi kwa tahadhari wakati wa misimu ya mvua kwa kipindi cha miaka mitano.