Ushahidi dhidi ya Joseph Kony waanza kuwasilishwa ICC
Waendesha mashtaka katika mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), wameanza kuwasilisha ushahidi dhidi ya kiongozi wa kundi la LRA Joseph Kony ambaye wapiganaji wake walisababisha mauaji makubwa na mateso kwa waakazi wa Kaskazini mwa Uganda.
Waendesha mashtaka wamewaambia na kuwaonesha majaji wanaosikiliza kesi hiyo jijini Hague, namna Joseph Kony na kundi lake walivyosababisha maumivu na hofu miongoni mwa watu, na kuwasababishia uoga mpaka sasa.
Wakili anayewawakilisha wahanga wa Sarah Pellet awemeka bayana mateso waliyoyapitia raia wa Uganda ambapo Kony anakabiliwa na mashtaka 39 ya uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu.
Ingawa sheria za ICC zinakataza kusikilizwa kwa kesi kamili bila mshtakiwa kuwepo, waendesha mashtaka wanadai kuwa vikao ni muhimu ili kuhakikisha kesi inaweza kuendelea haraka iwapo Jospeph Kony hatimaye atakamatwa.
Majaji wa ICC huko The Hague jana Jumanne walichunguza makosa 39 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu dhidi ya Kony, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, ubakaji, utumwa wa ngono na wizi.
Wakiongozwa na mbabe wa kivita aliyeko mafichoni Joseph Kony, waasi wa LRA waliwatia hofu Waganda kwa takriban miaka 20 wakipigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni kutoka kambi za kaskazini mwa Uganda na nchi jirani. Wanamgambo hao wameangamizwa kwa kiasi kikubwa, lakini Kony anasalia kuwa mmoja wa watoro wanaosakwa sana na mahakama ya ICC.
Genge la Kikristo na la kigaidi la LRA lilianzishwa na Mkatoliki Joseph Kony miongo mitatu iliyopita ambapo Kony alijiita pia nabii.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kundi hilo liliwauwa zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 waliolazimishwa kuwa watumwa wa ngono na askari vitani.