Indhari ya UN: Mafuriko makubwa Sudan Kusini yaweza kuathiri zaidi ya watu milioni moja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130720-indhari_ya_un_mafuriko_makubwa_sudan_kusini_yaweza_kuathiri_zaidi_ya_watu_milioni_moja
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) limetoa tahadhari kali kuhusu mafuriko makubwa yanayoendelea nchini Sudan Kusini, likisema kuwa tayari yameathiri watu wapatao 273,000 mwaka huu, na huenda yakawaathiri zaidi ya milioni moja katika miezi ijayo.
(last modified 2025-09-12T22:57:18+00:00 )
Sep 12, 2025 22:57 UTC
  • Indhari ya UN: Mafuriko makubwa Sudan Kusini yaweza kuathiri zaidi ya watu milioni moja

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) limetoa tahadhari kali kuhusu mafuriko makubwa yanayoendelea nchini Sudan Kusini, likisema kuwa tayari yameathiri watu wapatao 273,000 mwaka huu, na huenda yakawaathiri zaidi ya milioni moja katika miezi ijayo.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva, Mwakilishi wa UNHCR nchini Sudan Kusini, Marie-Hélène Verney, alisema: “Sudan Kusini inakumbwa tena na mafuriko makubwa, hususan katika maeneo ambayo yameathiriwa na mapigano mapya ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita.”

Verney alieleza kuwa idadi ya walioathirika imeongezeka mara tatu ndani ya mwezi Agosti pekee, huku takriban watu 100,000 wakilazimika kuhama makazi yao. Aliongeza kuwa: “Ikiwa hali hii itaendelea, tunakadiria kuwa zaidi ya watu milioni moja wataathirika katika miezi ijayo, ambapo 400,000 kati yao watahama makazi.” Mvua za mwaka huu zimeripotiwa kuwa nzito zaidi kuliko zile za mwaka uliopita.

Maeneo mazima ya majimbo ya Jonglei na Unity yameripotiwa kuzama chini ya maji, ikiwemo mashamba, mifugo, makazi ya watu, shule na vituo vya afya. Verney alionya kuwa mafuriko haya yanatokea sambamba na migogoro ya kijamii, uhaba wa chakula, na mlipuko wa kipindupindu uliowaathiri takriban watu 90,000.

UNHCR imetangaza kuwa inatoa kipaumbele kwa kuwasaidia watu wapatao 150,000, kwa kuwapatia msaada wa kifedha, makazi ya dharura, vifaa vya misaada kwa waliopoteza makazi, pamoja na hatua za ulinzi kwa walio hatarini.

Verney alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kifedha, akionya kuwa: “Bila ufadhili wa ziada, uwezo wetu wa kutoa makazi, ulinzi, na maji safi utabaki kuwa mdogo sana.”