Burkina Faso yatangaza viza bila malipo kwa Waafrika wote
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130726-burkina_faso_yatangaza_viza_bila_malipo_kwa_waafrika_wote
Burkina Faso imetangaza kuwa viza ya kuingia nchini humo kwa raia wote wa nchi za Afrika sasa itakuwa bila malipo, ikiwa ni sehemu ya hatua kadhaa zilizopitishwa na Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha kila wiki kilichoongozwa na Rais wa Mpito, Kapteni Ibrahim Traoré.
(last modified 2025-09-12T22:58:54+00:00 )
Sep 12, 2025 22:58 UTC
  • Burkina Faso yatangaza viza bila malipo kwa Waafrika wote

Burkina Faso imetangaza kuwa viza ya kuingia nchini humo kwa raia wote wa nchi za Afrika sasa itakuwa bila malipo, ikiwa ni sehemu ya hatua kadhaa zilizopitishwa na Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha kila wiki kilichoongozwa na Rais wa Mpito, Kapteni Ibrahim Traoré.

Msemaji wa serikali, Pingdwendé Gilbert Ouédraogo, alieleza Alhamisi kuwa uamuzi huo ni sehemu ya maono ya Uafrika wa Kapteni Traoré. “Kuanzia sasa, raia yeyote kutoka nchi ya Afrika anayetaka kuingia Burkina Faso hatalipa chochote kwa ajili ya ada ya viza,” alisema Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana.

Kwa mujibu wa Sana, agizo hilo linakusudia “kuimarisha uhuru wa kusafiri kwa watu wa Afrika na bidhaa zao ndani ya ardhi ya Burkina Faso, na pia kuchochea mshikamano wa bara.”

Hata hivyo, alifafanua kuwa mpango huo “haumaanishi kuondolewa sharti la viza.”

Kwa hatua hii, Burkina Faso imejiunga na Kenya, Ghana, Rwanda, Shelisheli, Gambia, na Jamhuri ya Benin katika kutoa fursa ya kuingia bila viza kwa wamiliki wa pasipoti za Afrika. Kuanzia Januari mwaka huu, serikali ya Kenya ilitangaza kuwa raia wa karibu nchi zote za Afrika sasa wataweza kuingia nchini humo bila kuhitaji kibali cha awali cha kusafiri.

Rwanda nayo inaruhusu raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola (Commonwealth), kupata viza bila malipo mara wanapowasili nchini humo, kwa ziara ya hadi siku 30.

Aidha, raia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaweza kuppata kibali cha kuingia Rwanda bila malipo kwa muda wa miezi sita, mara tu wanapowasili Rwanda.