Pendekezo la Saudi Arabia, UAE na Misri kuhusu 'Ramani ya Amani' ya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130754-pendekezo_la_saudi_arabia_uae_na_misri_kuhusu_'ramani_ya_amani'_ya_sudan
Ijumaa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri na pia Marekani zilitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda wa miezi mitatu nchini Sudan sambamba na kufanyika mazungumzo ya makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita.
(last modified 2025-09-13T08:21:50+00:00 )
Sep 13, 2025 08:21 UTC
  • Pendekezo la Saudi Arabia, UAE na Misri kuhusu 'Ramani ya Amani' ya Sudan

Ijumaa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri na pia Marekani zilitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda wa miezi mitatu nchini Sudan sambamba na kufanyika mazungumzo ya makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita.

Mataifa hayo manne yanachukuliwa kuwa na ushawishi katika Jeshi la Kitaifa la Sudan na kikosi cha waasi cha Rapid Support Forces (RSF), ambacho kilianzisha vita vilivyosababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani na kusambaza njaa.

Katika ramani ya amani iliyowasilishwa, mawaziri wa nchi hizo wametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja na kuanzishwa mchakato wa mpito wa miezi tisa kuelekea utawala wa kiraia unaoongozwa na raia wa Sudan.

Taarifa iliyotolewa na mawaziri hao wanne imesema. “Tunaamini kuwa hakuna suluhisho la kijeshi linalowezekana kwa mgogoro huu, na hali ya sasa inaleta mateso yasiyokubalika pamoja na hatari kwa amani na usalama wa kikanda.”

Jeshi la Sudan na RSF hawakutoa majibu ya haraka kuhusu pendekezo hilo.

UAE, mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo hilo, imetuhumiwa na jeshi la taifa la Sudan kwa kuunga mkono waasi wa RSF, tuhuma ambazo imezikanusha mara kadhaa. Waasi wa RSF wanatuhumiwa kwa kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita. Misri, na kwa kiwango kidogo Saudi Arabia, ni waungaji mkono wa Jenerali Abdul Fattah al-Burhan, kamanda mkuu wa jeshi ambaye anashikilia uongozi wa muda nchini Sudan.

Nchi hizo nne pia zimesisitiza kuunga mkono umoja wa Sudan, wakati ambapo RSF imeunda serikali mbadala. RSF inadhibiti sehemu kubwa ya eneo la Darfur, ambalo limekuwa ngome ya serikali hiyo ya mbadala.

Hadi sasa, waasi wa RSF wanaoongozwa na Hamdan Dagalo wanaendelea kupambana na jeshi la Sudan katika mji wa kihistoria wa al-Fashir, mji mkuu wa zamani wa Darfur, ambapo wameweka mzingiro mkali unaoendelea kusababisha njaa kwa wakazi wa mji huo.

Haijulikani iwapo pande zinazopigana zitakubali pendekezo la nchi hizo kuhusu ramani ya amani. Mnamo Juni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa wiki moja katika mji wa al-Fashir, wito ambao ulipokelewa na jeshi lakini ukakataliwa na waasi wa RSF.