Misri yaionya Israel kuhusu njama za kuwaua viongozi wa Hamas ndani ya ardhi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130756-misri_yaionya_israel_kuhusu_njama_za_kuwaua_viongozi_wa_hamas_ndani_ya_ardhi_yake
Misri imefichua njama za Israel za kuwaua viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, walioko ndani ya ardhi yake, na kuionya Israel kuwa shambulio lolote la aina hiyo litachukuliwa kama “tamko la vita” na litajibiwa kwa nguvu.
(last modified 2025-09-13T08:27:27+00:00 )
Sep 13, 2025 08:27 UTC
  • Misri yaionya Israel kuhusu njama za kuwaua viongozi wa Hamas ndani ya ardhi yake

Misri imefichua njama za Israel za kuwaua viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, walioko ndani ya ardhi yake, na kuionya Israel kuwa shambulio lolote la aina hiyo litachukuliwa kama “tamko la vita” na litajibiwa kwa nguvu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Middle East Eye (MEE) iliyotolewa Ijumaa, chanzo cha juu cha usalama kimeonya kuwa shambulio lolote la Israel dhidi ya viongozi wa Hamas walioko Misri litakuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya taifa hilo, na Cairo “haitasita” kuchukua hatua kali.

Taarifa hiyo imesema: “Ripoti za kiintelijensia zinaashiria kuwa Israel imekuwa ikipanga kwa muda mrefu kuwaua viongozi wa Hamas walioko Cairo, na Misri tayari ilizima jaribio moja wakati wa mazungumzo ya kusitisha mapigano yaliyofanyika jijini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.”

Afisa hiyo wa usalama ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema:

“Jaribio lolote dhidi ya maisha ya viongozi wa Hamas ndani ya ardhi ya Misri litachukuliwa kama uvunjaji wa mamlaka ya kitaifa, na hivyo basi tamko la vita kutoka Israel, ambalo hatutasita kulijibu kwa nguvu."

Ingawa hakujathibitishwa rasmi kuwa viongozi wa juu wa Hamas wanaishi Misri, chanzo hicho kilieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakiishi nchini humo kwa miaka mingi, hata kabla ya kuanza vita vya sasa vya Gaza, huku majina yao, idadi na maeneo yao yakibaki siri kwa sababu za kiusalama.

Viongozi wa Misri, kwa mujibu wa chanzo hicho, wameihimiza Israel kurejea kwenye meza ya mazungumzo na kutafuta njia ya kusitisha mapigano Gaza, badala ya kuendeleza mzunguko wa vita visivyoisha na kuchochea mvutano wa kikanda.

Ripoti ya Middle East Eye pia ilinukuu mchambuzi mmoja wa usalama akisema, “Uwezo wa Misri kuwa mpatanishi wa kuaminika katika mgogoro wa Gaza utaporomoka endapo Israel itaruhusiwa kufanya mauaji ya kisiasa ndani ya Cairo bila kudhibitiwa.”

Haye yameripotiwa baada ya utawala wa Israel kushambulia majengo ya makazi katika mji mkuu wa Qatar, Doha, Jumanne, yakilenga Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, viongozi wake, pamoja na raia kadhaa wa Qatar. Maafisa kadhaa wa Hamas na raia wa Qatar waliuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi.

Mashambulizi hayo yamezua hofu na kulaaniwa vikali duniani kote, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akionya kuwa Tel Aviv itaendelea kuwashambulia viongozi wa Hamas walioko katika mataifa mengine.