Rwanda yaikemea Ulaya kwa 'kuingilia haki' kwa kutaka Victoire Ingabire aachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130882-rwanda_yaikemea_ulaya_kwa_'kuingilia_haki'_kwa_kutaka_victoire_ingabire_aachiliwe_huru
Bunge la Rwanda limetoa tamko kali likilaani azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) linalotaka kuachiwa huru mwanasiasa wa upinzani, mwanamama Victoire Ingabire.
(last modified 2025-09-16T22:49:04+00:00 )
Sep 16, 2025 22:49 UTC
  • Rwanda yaikemea Ulaya kwa 'kuingilia haki' kwa kutaka Victoire Ingabire aachiliwe huru

Bunge la Rwanda limetoa tamko kali likilaani azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) linalotaka kuachiwa huru mwanasiasa wa upinzani, mwanamama Victoire Ingabire.

Bunge la Rwanda limesema, azimio hilo la Bunge la Umoja wa Ulaya ni “kuingilia uhuru wa mfumo wa haki nchini Rwanda.”

Katika kikao cha pamoja cha mabaraza yake yote mawili Baraza la Wawakilishi na Seneti, Bunge la Rwanda limesema kuwa, hatua hiyo inakiuka misingi ya kimataifa ya uhuru wa mahakama na demokrasia.

Mnamo Septemba 11, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipitisha azimio likiitaka serikali ya Rwanda kumuachilia huru mara moja na bila masharti Victoire Ingabire pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani wanaoshikiliwa kwa kile walichokiita kutekeleza haki zao za msingi kwa amani. Aidha, walitaka mashtaka ya kisiasa dhidi yao yafutwe.

Ingabire, ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha DALFA–Umurinzi (ambacho bado hakijasajiliwa rasmi nchini Rwanda), alikamatwa mnamo Juni 19 mwaka huu na Ofisi ya Upelelezi wa Rwanda (RIB).

Kulingana na RIB, hatua hiyo ilifuatia maelekezo ya Mwendesha Mashtaka aliyelitaka shirika hilo kutekeleza agizo la Mahakama Kuu, kwa lengo la kumfikisha mahakamani.

Mahakama ilikuwa haijaridhika na maelezo aliyotoa kuhusiana na wafuasi wake wanaotuhumiwa kujaribu kupindua serikali.

Ingabire anakabiliwa na mashtaka sita, yakiwemo ya kujihusisha na kundi lenye nia ya kuangusha serikali, madai anayoyakana vikali.

Bunge la Rwanda limetaja azimio la Bunge la EU kuwa “limejengwa juu ya taarifa zenye upendeleo na zisizo sahihi,” ambazo zimeenezwa na wanasiasa walioko nje wanaopinga uongozi wa Rwanda, kwa lengo la kudhoofisha taasisi huru zilizojengwa juu ya misingi ya demokrasia, maendeleo, na heshima ya Rwanda kimataifa.