Ripoti: Rushwa iliyokithiri inatishia ustawi wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130884-ripoti_rushwa_iliyokithiri_inatishia_ustawi_wa_sudan_kusini
Tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, imetoa wito kwa idara za uchunguzi kuchunguza tuhuma za rushwa na utakatishaji fedha ambao unatishia ustawi wa nchi hiyo.
(last modified 2025-09-16T22:49:27+00:00 )
Sep 16, 2025 22:49 UTC
  • Ripoti: Rushwa iliyokithiri inatishia ustawi wa Sudan Kusini

Tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, imetoa wito kwa idara za uchunguzi kuchunguza tuhuma za rushwa na utakatishaji fedha ambao unatishia ustawi wa nchi hiyo.

Aidha tume hiyo, imesema hali ya rushwa na ubadhilifu wa fedha za uma nchini humo imefikia hatua mbaya ambayo inaweza kuitumbukiza tena nchi hiyo kwenye mzozo mwingine wa kisiasa. Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamewatuhumu viongozi wa Sudan Kusini, kwa kupora mali ya nchi hiyo.

Miongoni mwa uporaji uliotajwa ni kulipa dola bilioni 1.7 kwa makampuni yanayohusishwa na Makamu wa Rais Benjamin Bol Mel kwa ujenzi wa barabara ambayo haijawahi kufanyiwa kazi yoyote.

Kwa mujibu wa wa mwenyekiti wa tume hiyo, Yasmin Sooka, uchunguzi wao umebaini ofisi ya Rais Salva Kiir kutumia kiwango kikubwa cha fedha kuliko hata bajeti inayotolewa kwenye wizara.

Sook ameongeza kuwa, kati ya mapipa ghafi ya mafuta yanayopatikana kwenye taifa hilo, ni pipa moja tu ndilo linaingia kwenye mfuko wa serikali, akihoji ni wapi mapipa 39 yanapelekwa.

Kwa upande wake, mjumbe wa tume iliyochunguza hali ya rushwa kwenye taifa hilo, Barney Afako, uteuzi wa upendeleo katika nafasi za juu serikalini, ikiwemo kupandishwa vyeo kiholela kwa majenerali wa jeshi, kumechangia hali kuwa mbaya.

Afako ametolea mfano fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazounganisha mji mkuu wa Juba, kuwa ni barabara moja pekee ambayo inaelekea kukamilika katik ya tatu zilizokuwa zijengwe awali, huku fedha zilizotengwa zikiwa hazijulikani zilikopelekwa.