Wamalawi wasubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi wa urais
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Malawi huku raia wakisubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi wa urais na wa bunge uliofanyika hivi karibuni.
Wagombea takriban 17 wanachuana katika kinyang’anyiro cha urais, ambapo Rais Lazarus Chakwera anatafuta muhula wa pili huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mtangulizi wake, Peter Mutharika.
Matokeo kutoka vituo vya kupigia kura yanapelekwa katika vituo vya majimbo kwa ajili ya kujumlishwa kabla ya kutumwa katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Malawi (Malawi News Agency), vyombo vya habari vya ndani vimeruhusiwa kutangaza matokeo ya awali kutoka vituoni, ingawa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) imeelekeza kuwa takwimu hizo lazima zihakikiwe na maafisa wa tume kabla ya kutangazwa rasmi.
Jaji Annabel Mtalimanja, Mwenyekiti wa MEC, amenukuliwa akisema: “Tume ya Uchaguzi ya Malawi inaruhusu vyombo vya habari kutangaza matokeo ya awali viliyokusanya, lakini ni lazima vihakikishe kuwa takwimu hizo zimethibitishwa na maafisa wa tume kabla ya kutangaziwa umma.”
Waangalizi wa uchaguzi wamesema ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi wa urais unahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, hali inayofanya duru ya pili ya uchaguzi kuwa na uwezekano mkubwa, ambayo inapaswa kufanyika ndani ya siku 60.
Mambo yaliyojitokeza sana katika fikra za wapiga kura ni mfumuko wa bei na gharama kubwa za chakula. Malawi imekumbwa na hali ya kudorora kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni, huku kimbunga kikubwa na ukame wa kikanda vikisababisha mazao kuharibika na kuongeza ugumu wa maisha.
Nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 22 pia ilifanya uchaguzi wa wabunge na madiwani siku ya Jumanne.