Mutharika aongoza kwa kishindo katika kinyang’anyiro cha urais nchini Malawi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131166-mutharika_aongoza_kwa_kishindo_katika_kinyang’anyiro_cha_urais_nchini_malawi
Rais wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika, ameibuka na uongozi wa kishindo katika hesabu za kura za uchaguzi wa urais, akijikusanyia takriban asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa.
(last modified 2025-09-24T02:14:42+00:00 )
Sep 24, 2025 02:14 UTC
  • Mutharika aongoza kwa kishindo katika kinyang’anyiro cha urais nchini Malawi

Rais wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika, ameibuka na uongozi wa kishindo katika hesabu za kura za uchaguzi wa urais, akijikusanyia takriban asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa.

Matokeo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) kufikia Jumanne yanaonyesha kuwa Rais aliyeko madarakani, Lazarus Chakwera, amepata asilimia 24 pekee ya kura, hali inayodhihirisha mabadiliko makubwa ambapo Mutharika ameonyesha ufanisi hata katika maeneo yaliyokuwa ngome ya mpinzani wake.

MEC inatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho leo Jumatano, kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 16 Septemba.

Takriban wilaya 12 bado hazijatangaza matokeo, zikiwemo maeneo ya vijijini karibu na Lilongwe na Dedza ambako kambi ya Chakwera inatarajia kurejesha uungwaji mkono.

Wilaya mbili ambako Mutharika anatarajiwa kupata ushindi mkubwa zimezuia kwa muda kutangaza matokeo yao hadi uhakiki utakapokamilika.

Mgombea anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kuepuka duru ya pili ya uchaguzi.

Kambi ya Chakwera imeitaka kufanyike “ukaguzi wa kimwili” wa matokeo, ikidai kuwepo kwa dosari ambazo hazijafafanuliwa.

Polisi wamewakamata waandishi wa data wanane wanaoshukiwa kujaribu kubadilisha takwimu za kura.

Tume hiyo imeahidi uwazi na usahihi, ikikumbuka mgogoro wa uchaguzi wa mwaka 2019 ambapo ushindi wa awali wa Mutharika ulifutwa na mahakama ya katiba kutokana na kasoro mbalimbali.

Chakwera alishinda kwa kishindo katika marudio ya uchaguzi mwaka 2020, lakini utawala wake umekumbwa na misukosuko ya kiuchumi ikiwemo mfumuko mkubwa wa bei, uhaba wa mafuta, na kukatika kwa umeme mara kwa mara.