Waandamanaji nchini Morocco: Tunahitaji zaidi hospitali kuliko viwanja vya soka
Makabiliano makali yanaripotiwa kutokea baina ya waandamanaji na vyombo vya usalama nchini Morocco.
Maandamano yanaendelea nchini Morocco hukuwananchi wakiushinikiza utawala ulioko madarakani kutekeleza mageuzi kuhusu namna huduma zinavyotolewa kwa wananchi, lakini pia kumaliza suala la ufisadi.
Morocco kwa sasa inajenga kile kitakachokuwa uwanja mkubwa zaidi wa soka duniani kwa ajili ya maandalizi ya kuandaa Kombe la Dunia la 2030.
Lakini kwa waandamanaji ambao wameingia mitaani kila usiku nchini kote tangu Jumamosi iliyopita wanalalamikia miundombinu mingine yote ya kandanda inayoendelea kujengwa kwa gharama ya dola bilioni 5. Wanasema kuwa hiyo ni dharau kwa wananchi wa Morocco kwa sababu serikali imeshindwa kutoa kipaumbele kwa mahitaji muhimu kwa wananchi.
" Ninaandamana kwa sababu nataka nchi yangu iwe bora. Sitaki kuondoka Morocco, na sitaki kuichukia nchi yangu alisikika akisema Hajar Belhassan, meneja mawasiliano mwenye umri wa miaka 25 kutoka Settat, umbali wa kilomita 80 (maili 50) kusini mwa Casablanca.
Kundi kwa jina la Gen Z 212 namba inayotumika katika msimbo wa kimataifa wa upigaji simu huko Morocco limekuwa imekuwa likiratibu maandamano kupitia jukwaa la michezo ya kubahatisha na vile vile kupitiaTikTok na Instagram.
Vijana wa Morocco ambao wamepata msukumo kufuatia maandamano ya karibuni ya Gen-Z huko Nepal wanawataka viongozi wa serikali kuchukua hatua haraka na kwa ari kushughulikia matatizo mbalimbali ya wananchi sawa kabisa na walivyofanya katika kadhia hii ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya dunia.