Mto Nile nchini Sudan wafurika, maji ya Blue na White Nile yaongezeka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131706-mto_nile_nchini_sudan_wafurika_maji_ya_blue_na_white_nile_yaongezeka
Mafuriko makubwa katika Jimbo la Mto Nile nchini Sudan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 30 na maelfu ya wengine kukwama. Wakazi wa eneo hilo wanaelezea jinsi walivyopitisha usiku wa hofu wakati mafuriko yalipopita katikati ya nyumba na mashamba yao.
(last modified 2025-10-07T09:58:41+00:00 )
Oct 07, 2025 09:58 UTC
  • Mto Nile nchini Sudan wafurika, maji ya Blue na White Nile yaongezeka

Mafuriko makubwa katika Jimbo la Mto Nile nchini Sudan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 30 na maelfu ya wengine kukwama. Wakazi wa eneo hilo wanaelezea jinsi walivyopitisha usiku wa hofu wakati mafuriko yalipopita katikati ya nyumba na mashamba yao.

Maafisa wa eneo hilo wamesema kuwa, mafuriko ya mito ya Blue na White Nile yameharibu mamia ya nyumba na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

"Tulishtushwa na mafuriko haya makubwa," amesema Ramadan Ali na kuongeza kwa kusema: "Tulikuwa tumelala na mwendo wa saa 7:30 usiku, mafuriko yalifika kwenye eneo letu. Tuliamka, hatukuweza kupata njia ya kukabiliana na kiasi kikubwa sana cha maji. Lakini kwa sasa tunajitahidi kuyaondoa. Hali yetu ni mbaya sana, naam, mbaya sana. Kila mtu hapa anateseka kwa sasa, huo ndio ukweli."

Ukosefu wa vifaa na uwekezaji umekwamisha mipango ya ndani ya kupunguza uharibifu wa mafuriko ya mara kwa mara huku mvua kubwa ikiendelea kukwamisha jitihada za uokoaji katika baadhi ya maeneo ya mabondeni.

Majimbo mengine yaliyokumbwa na mafuriko ni pamoja na Blue Nile, Gezira na Khartoum. Katika jimbo la Mto Nile, wakaazi wanasema janga hilo lingeweza kuepukika.

Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji ya Sudan hapo awali ilitangaza majina ya majimbo sita ambayo yalikuwa kwenye hatari kubwa ya mafuriko ya Mto Nile mwaka huu, ikiwa ni pamoja na Jimbo la Gezira na Khartoum. Maafisa wa serikali wamewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuchukua tahadhari zote muhimu.

Misri, ambayo pia imeshuhudia mafuriko katika Delta ya Nile, imeinyooshea kidole cha lawama Ethiopia ikidai kuwa bwawa la al Nahdha la Ethiopia ndilo lililosababisha maafa hayo.