Umoja wa Mataifa waeleza wasiwasi kuhusu machafuko kaskazini mwa Msumbiji
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi ulionao kuhusu idadi kubwa ya raia wanaokimbia machafuko yanayoendelea kaskazini mwa Msumbiji, ambapo wengi wao wamefikia hatua ya kukata tamaa.
Xavier Creach, mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Msumbiji amesema mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, wameshuhudia mateso makubwa huku raia wa kawaida wakilengwa moja kwa moja na mashambulizi.
Shirika hilo limeripoti kuwa zaidi ya watu 100,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu, huku watu 22,000 walikimbia ndani ya wiki moja tu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba.
Mashambulizi mapya yameripotiwa katika miezi ya hivi karibuni katika jimbo la Cabo Delgado, ambako uasi unaoendeshwa na makundi yenye mfungamano na kundi la Daes umeendelea tangu mwaka 2017.
Mwezi uliopita, waasi hao walishambulia bandari muhimu ya Mocimboa da Praia, wakipambana na vikosi vya serikali na kuwachinja raia, tukio lililozua hofu kubwa na kusababisha kuongezeka idadi ya wakimbizi wa ndani.
Kiwango kikubwa cha gesi asilia kiligunduliwa katika eneo la Cabo Delgado mwaka 2010. Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la kigaidi la DAESH walianzisha uasi mkoani humo mwama 2017 na kusitisha uchimbaji wa gesi hiyo. Imeelezwa kuwa watu wapatao 5,800 wameuawa katika machafuko na mapigano yaliyosababishwa na kundi hilo.
Kampuni ya TotalEnergies, ambayo ilisitisha mradi huo mkubwa wa uchimbaji gesi baada ya mashambulizi ya 2021 ambapo watu kadhaa waliuawa, imetangaza kuwa mradi huo utaanza tena mwaka huu pale "amani na usalama" vitakaporejea huko Cabo Delgado.