Amnesty International yaitaka Nigeria kuwaondoa hatiani wanaharakati tisa waliouawa miaka 30 iliyopita
-
Vinara wa maandamano ya Ogoni Nine
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Nigeria kuwafutia kabisa hatia wanaharakati tisa wa mazingira waliouawa miaka 30 iliyopita, ambao walipigania kulinda eneo la Niger Delta kutokana na shughuli za kampuni kubwa ya mafuta ya Shell.
Wito huu umetolewa sambamba na maadhimisho ya miaka 30 baada ya serikali ya Nigeria kuwanyongwa wanaharakati tisa maarufu wa mazingira wanaojulikana kama "Ogoni Nine," - kitendo ambacho shirika hilo limekitaja kuwa cha "kikatili"-. Kumbukumbu ya mauaji hayo mwaka huu imesadifiana na kuanza Mkutano wa Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa nchini Brazil.
Maandamano ya Ogoni Nine ya mwaka 1995 yalielekeza macho ya walimwengu kwenye maafa yanayosababishwa na tasnia ya nishati ya visukuku kwenye hali ya hewa, maisha ya binadamu na mazingira, na katika kuendelea umaskini katika maeneo yanayozalisha mafuta.
Mwezi Juni mwaka huu, serikali ya Nigeria ilitoa msamaha kwa Ogoni Nine. Ingawa Amnesty International ilikaribisha hatua hiyo, lakini iliitaja kuwa haitoshi kutimiza haki kwa wanaume hao walionyongwa na serikali na kwa familia zao.
Mkurugenzi wa tawi la Amnesty International nchini Nigeria, Isa Sanusi alisema: "Ingawa msamaha huu ni hatua moja mbele, lakini wanaharakati hao tisa wanastahili kuondolewa hatia kikamiilifu," na kuongeza kuwa: "Watu hawa waliuawa kidhulma kwa kosa ambalo hawakulifanya, na familia zao zimeteseka vya kutosha na zinastahili kutendewa uadilifu."
Sanusi alieleza kwamba wanaharakati hao tisa (Ogoni Nine), wakiongozwa na mwandishi na mwanaharakati Ken Saro-Wiwa, waliuawa kikatili mwaka wa 1995 na "utawala wa kijeshi uliotaka kuficha uhalifu wa kampuni ya Shell na makampuni mengine ya mafuta ambao ulikuwa umeharibu maisha na riziki ya makumi ya maelfu ya wakazi wa Niger Delta kutokana na kumwagika na kuvuja mara kwa mara kwa mafuta."