Rais wa Niger: Ufaransa inatekeleza njama za kuvuruga nchi yake
Rais wa Niger, Abdourahamane Tchiani, ameishutumu vikali Ufaransa kwa kuhusika katika njama za kuichafua na kuidhoofisha nchi yake.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika mkoa wa Tahoua, magharibi mwa Niger, Rais Tchiani alikemea kile alichokiita kuingilia kwa nguvu nchi za kibeberu, akisema: “Nguvu za ukoloni, hususan Ufaransa, zinawatumia raia wa Niger kushambulia miundombinu muhimu ya taifa.”
Aidha, amelaani “matendo ya baadhi ya raia wa taifa hilo ambao, kwa kushirikiana au kwa mienendo ya kupotoka, wanajaribu kuleta machafuko nchini.”
Rais Tchiani alisisitiza kuwa njama hizo hazitafaulu, akieleza: “Wale wanaojificha nyuma ya dini ili kutekeleza uhalifu wao si chochote ila ni wezi na wahuni waliopotoshwa.”
Ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kumkosoa Ufaransa. Mnamo mwezi Juni, aliituhumu Paris na washirika wake kwa kupanga njama za kuisambaratisha JMuungano wa Mataifa ya Sahel (AES) kupitia mitandao ya siri, makundi yenye silaha, na wafuasi wa kikanda.
Muungano huo ulianzishwa rasmi Septemba 2023 na Burkina Faso, Mali, na Niger kama mkataba wa pamoja wa ulinzi na ushirikiano baada ya kutimuliwakwa wanajeshi wa Ufaransa katika mataifa hayo. Tangu wakati huo, nchi hizo zinazoongozwa na serikali za mpito za kijeshi zimejiondoa kutoka jumuiya ya ECOWAS, zikiitaja kuwa chombo cha ushawishi wa mkoloni wa zamani, Ufaransa, na tishio kwa uhuru wao; na pia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusema mahakama hiyo ni chombo cha ubeberu cha "Ukoloni Mamboleo".
Hivi karibuni Jenerali Tchiani alitangaza kuwa viongozi wa AES wamedhamiria "kuunda na kuimarisha kikosi cha kijesi kilichounganishwa ambacho wakuu wake watafanya kazi kwa pamoja."
Ikumbukwe kuwa, Julai mwaka huu, Muungano wa Mataifa ya Sahel, AES, ulitangaza uzinduzi wa kadi ya utambulisho (kitambulisho) ya pamoja inayotumia teknolojia ya kibiometri.