Hamas yakataa mpango wa vikosi vya kigeni Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133278-hamas_yakataa_mpango_wa_vikosi_vya_kigeni_gaza
Makundi ya Kipalestina yakiongozwa na Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Palestina, Hamas, yamepinga vikali mpango wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kupeleka vikosi vya kigeni  katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-11-17T09:11:05+00:00 )
Nov 17, 2025 09:11 UTC
  • Hamas yakataa mpango wa vikosi vya kigeni Gaza

Makundi ya Kipalestina yakiongozwa na Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Palestina, Hamas, yamepinga vikali mpango wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kupeleka vikosi vya kigeni  katika Ukanda wa Gaza.

Makundi hayo yameitaka Algeria, mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza hilo, kusimama imara dhidi ya pendekezo hilo.

Azimio la rasimu, linalotarajiwa kupigiwa kura leo Jumatatu, linapendekeza kupelekwa karibu wanajeshi 20,000 wa kigeni wenye mamlaka ya kutumia nguvu, kudhibiti mipaka ya Gaza, kufundisha polisi wa Kipalestina, na kusimamia mpango wa kuondoa silaha.

Katika tamko la pamoja, makundi hayo yamelaani mpango huo wakisema ni “jaribio jipya la kulazimisha aina nyingine ya ukaliaji wa mabavu katika ardhi na watu wetu, na kuhalalisha uangalizi wa kigeni.”

Aidha makundi hayo ya kupigania ukombozi wa Palestina yamebaini kuwa: “Tunatoa wito wa dhati na wa kindugu kwa Jamhuri ya Algeria, serikali na wananchi wake, kuendelea kushikilia misimamo yake ya kimsingi ya kuunga mkono Palestina, na msimamo wake thabiti wa kukataa miradi yoyote inayolenga kuvuruga utambulisho wa Gaza na haki ya watu wetu ya kujitawala.”

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, amesisitiza kuwa marekebisho yaliyomo katika rasimu ya Marekani “hayaleti uthabiti Gaza.” Amekumbusha kuhusu msimamo wa Wapalestina kwamba wanahitaji azimio la Baraza la Usalama litakalolinda haki yao ya kujitawala na kuzuia vita dhidi ya Ukanda huo.

Maher al Taher wa Chama cha Ukombozi wa Umma wa Palestina alionya kuwa hatari ya mpango huo “iko katika kugeuza Ukanda wa Gaza kuwa eneo lisilo chini ya utawala wa Kipalestina,” kwa kipindi cha mpito “kinachoweza kudumu kwa miaka mingi, jambo linaloweka hatari kubwa na kuendeleza aina mpya ya ukaliaji wa mabavu.”