Ajali ya mgodi yaua watu 32 nchini DRC
Daraja la mgodi wa kobalti kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limeporomoka na kuua wachimbaji wasiopungua 32, afisa wa serikali ya mkoa alithibitisha Jumapili.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi katika eneo lenye mafuriko kwenye mgodi wa Lualaba. Waziri wa mambo ya ndani wa mkoa huo, Roy Kaumba Mayonde, amesema miili 32 imepatikana na jitihada za uokoaji zinaendelea.
DRC huzalisha zaidi ya asilimia 70 ya kobalti duniani, madini muhimu kwa betri za magari ya umeme, kompyuta na simu za mkononi. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 200,000 wanajihusisha na uchimbaji haramu wa kobalti katika taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati.
Mamlaka za eneo zilisema daraja liliporomoka katika mgodi wa Kalando, takribani kilomita 42 kusini mashariki mwa Kolwezi, makao makuu ya mkoa wa Lualaba.
Mayonde alieleza kuwa: “Licha ya marufuku rasmi ya kuingia mgodini kutokana na mvua kubwa na hatari ya maporomoko, wachimbaji haramu waliingia kwa lazima.” Aliongeza kuwa daraja la muda lililojengwa kuvuka mtaro uliojaa maji lilibomoka baada ya wachimbaji kulikimbilia kwa wingi.
Ripoti ya shirika la serikali SAEMAPE, linalosimamia vyama vya wachimbaji, ilisema uwepo wa askari katika mgodi wa Kalando ulisababisha hofu. Mgodi huo umekuwa kitovu cha mzozo wa muda mrefu kati ya wachimbaji, chama cha ushirika kilichokusudiwa kuratibu uchimbaji, na waendeshaji halali wa mgodi wanaohusishwa na wawekezaji wa Kichina.
Picha zilizotumwa na ofisi ya tume ya kitaifa ya haki za binadamu (CNDH) mkoani zilionyesha wachimbaji wakichimba miili kutoka kwenye mtaro, huku angalau miili 17 ikiwa imetandazwa ardhini.
Mratibu wa CNDH mkoani, Arthur Kabulo, alisema zaidi ya wachimbaji haramu 10,000 hufanya kazi katika mgodi wa Kalando. Mamlaka za mkoa zilisitisha shughuli za mgodi huo Jumapili.
Utajiri wa madini wa DRC pia umekuwa chanzo cha mizozo iliyolikumba eneo la mashariki mwa nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu.