Save the Children: Homa ya manjano DRC kusambaa duniani kote
Shirika la kimataifa la Save the Children limeonya kuwa, mripuko wa homa ya manjano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yumkini ukasambaa katika nchi mbali mbali duniani, iwapo Jamii ya Kimataifa itaendelea kupuuza suala la chanjo ya ugonjwa huo.
Heather Kerr, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo huko Kongo DR amesema kutokana na kutokuwa na tiba homa ya manjano na utengenezaji chanjo yake kuwa unachukua muda wa mwaka mzima, huenda mripuko wa ugonjwa huo ukaenea kote duniani iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, kuna akiba ya chanjo milioni 7 tu za dharura za homa ya manjano, jambo ambalo linaiweka dunia na hususan nchi nyingi zinazopakana na DRC katika hatari ya kushuhudia maambukizi ya maradhi hayo.
Shirika la Afya Duniani WHO limesema linapania kutoa chanjo hiyo kwa watu milioni 8.5 katika mji mkuu wa Kongo DR Kinshasa na kwa watu milioni 3.4 katika maeneo ya mipaka ya nchi hiyo.
Mwezi uliopita, WHO ilisema kuwa kesi za maambukizi mapya ya ugonjwa hatari wa homa ya manjano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeongezeka kwa asilimia 38 katika kipindi cha wiki tatu. Kesi nyingi za ugonjwa huo zimehusishwa na mripuko wa homa ya manjano katika nchi jirani ya Angola ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 350 tangu mwezi Disemba mwaka jana.
Aidha shirika hilo la afya duniani lilisema kuwa ugonjwa wa homa ya manjano ulioripuka nchini Angola sasa umeenea sio tu katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, bali pia Kenya na China.