Maandamano Nigeria kushinikiza kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
Kwa mara nyingine tena maelfu ya wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano katika mji wa Bauchi, kaskazini mashariki mwa nchi, kushinikiza kuachiwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Waandamanaji hao aghalabu yao wakiwa wanawake walikuwa wamebeba mabango na maberamu yaliyobeba ujumbe wa kuitaka serikali ya Abuja imuachie huru mara moja msomi huyo wa Kiislamu, mkewe na mamia ya Waislamu wengine wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo. Maandamano mengine kama hayo jana Jumatatu yalifanyika katika mji wa Yauri, jimbo la Kebbi lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Alkhamisi iliyoita, Wanaharakati wapatao 200 wa Kiislamu waliokamatwa katika operesheni ya kikatili ya jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka jana walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria na kuvuruga amani. Itakumbukwa kuwa, Tarehe 12 hadi 14 Disemba mwaka uliopita wa 2015, jeshi la Nigeria lilishambulia kituo cha kidini na nyumba ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu wasio na hatia. Hatima ya Sheikh Zakzaky ambaye alipigwa risasi kadhaa katika hujuma hiyo, bado haijajulikana mpaka sasa.