ICC imemhukumu kiongozi wa Janjaweed wa Darfur kifungo cha miaka 20 jela
-
Ali Muhammad Ali Abdulrahman
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) leo Jumanne wamemhukumu kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed katika jimbo la Darfur Sudan kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ukatili katika jimbo la Darfur.
Ali Muhammad Ali Abdulrahman anayejulikana pia kama Ali Kushayb, alitiwa hatiani mwezi Oktoba mwaka huu kwa makosa 27 ya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu yakiwemo mauaji, utesaji na vitendo vya ubakaji na ukatili mwingine uliotekelezwa na wanamgambo wa Janjaweed katika machafuko ya Darfur zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Katika kesi iliyosikilizwa mwezi uliopita, waendesha mashtaka wa mahakama ya ICC yenye makao yake huko Hague Uholanzi walitaka Ali Muhammad Ali Abdulrahman ahukumiwe kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia mwezi Oktoba kwa makosa 27 ya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Ali Muhammad Abdulrhman aliyekuwa kinara wa wanamgambo wa Janjanjaweed miaka ishirini iliyopita huko Darfur amepatikana na hatia pia ya kuamuru kuuliwa watu kwa umati na kuwapiga kwa shoka hadi kufa wafungwa wawili kati ya mwaka 2003 na 2004.
Mwendesha Mashtaka katika mahakama ya ICC Julian Nicholls aliwaambia majaji katika kikao cha hukumu mwezi Novemba kwamba Ali Muhammad Ali Abdulrahman au Ali Kushayb alitenda jinai zote hizo kwa kwa kujua na kwa makusudi na upo ushahidi wa kuthibitisho hilo.
Ali Kushayb aliye na umri wa miaka 76 alisimama na kusikiliza, lakini hakuonyesha kuguswa na Jaji Kiongozi Joanna Korner alipotoa hukumu hiyo.