Algeria yaijia juu Ufaransa kwa kueneza 'urongo' kupitia TV
Serikali ya Algeria imeishutumu Ufaransa kwa kuidhinisha 'uchokozi' dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, baada ya televisheni ya serikali ya Paris kurusha makala ya matukio ya kweli (documentary) ambayo Algiers imesema imejaa "urongo na uzushi."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imemuita balozi mdogo wa Ufaransa huko Algiers kulalamikia kile ilichokieleza kuwa "matusi yaliyowasilishwa kama makala."
Imesema makala hiyo si kitu kingine ghairi ya msururu wa urongo unaopingana na uhalisia na ambao unakera sana, mbali na kuchochea hisia bila sababu za msingi.
Wizara hiyo imesema imemwonya mwanadiplomasia huyo wa Ufaransa kuhusu "uzito mkubwa" wa kuongezeka mienendo hasi mkoloni huyo wa zamani dhidi ya Algeria na kusisitiza kwamba, Algiers "ina haki ya kuchukua hatua zozote za ufuatiliaji ambazo uzito wa vitendo hivyo unaweza kuhitaji."
Alkhamisi iliyopita, runinga ya serikali ya France 2 ilirusha makala hiyo, chini ya anuani isemayo, ‘Uvumi na Mbinu Chafu: Vita vya Siri Kati ya Ufaransa na Algeria’, ikionyesha kampeni za siri za vitisho, ushawishi, na taarifa potofu zinazodaiwa kufanywa na mamlaka ya Algeria dhidi ya Ufaransa.
Haya yanajiri katika hali ambayo, Paris na Algiers zipo katika mvutano na mgogoro mkubwa wa kidiplomasia. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, Bunge la Algeria lilipasisha kwa kauli moja sheria inayotambua ukoloni wa Ufaransa nchini humo kuwa ni jinai, ikiutaja kuwa ni "uhalifu wa serikali," na kuitaka Ufaransa iombe msamaha rasmi kwa jinai hiyo.
Sheria ya kutambua ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuwa ni uhalifu inasisitiza kwamba "fidia kamili na yenye mlingano kwa uharibifu wote wa kimwili na kimaadili uliosababishwa na ukoloni wa Ufaransa ni haki ya msingi ya serikali na watu wa Algeria."