Sheikh Ibrahim Zakzaky apinga pendekezo la Trump kuhusu Gaza
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, amelitaja pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu makubaliano ya usitishaji vita kati ya Israel na Hamas kuwa ni “uoga”, hasa kutokana na sharti linalodaiwa la kuitaka Hamas kusalimisha silaha zake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Abuja, Nigeria, Sheikh Zakzaky alihoji sababu ya Israel kutaka Hamas iachane na silaha zake kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita.
Amesema: “Huu ni uoga. Unawezaje kupigana na adui kisha ukamtaka adui huyo aweke chini silaha zake, kama wewe si mwoga? Wazayuni wanataka tu kuua bila wao kuuawa.”
Sheikh Zakzaky ameongeza kuwa sharti hilo lina maana ya kutaka upande wa Palestina usalimishe silaha ili uwe rahisi kushambuliwa.
Amesema Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS haitasalimisha silaha zake kwa kisingizio chochote, lakini inaweza kukubali suluhisho litakalohusisha kuondolewa majeshi ya Israel kutoka maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa Sheikh Zakzaky, katika hali hiyo, upande wa muqawama unaweza kukubali kutoshambulia majeshi ya Israel wakati wa kujiondoa kwake. Hata hivyo, amesema hakuna mtu atakayekubali kukabidhi silaha zake kwa adui anayelenga kumuua.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria pia amesema kuwa kupinga dhulma ni jambo la kawaida kwa binadamu, na kwamba kuendelea mashambulizi ya Israel kutasababisha kuendelea muqawama wa Palestina.
Amesema, kila mara Israel itaakapotekeleza mashambulizi, bila shaka kutakuwa na muqawama akisisitiza kuwa muqawama huo si wa harakati moja pekee bali ni wa watu wa Palestina kwa ujumla ambao, kwa mujibu wake, hawataacha mapambano yao hadi kukombolewa ardhi zao kutokana mikononi mwa maghasibu.