EC yaonya wenye nia ya kuvuruga uchaguzi Uganda
(last modified Thu, 18 Feb 2016 02:12:25 GMT )
Feb 18, 2016 02:12 UTC
  • EC yaonya wenye nia ya kuvuruga uchaguzi  Uganda

Tume ya uchaguzi nchini Uganda imewaonya vikali wenye nia ya kuvuruga zoezi la upigaji kura linalofanyika leo (Alkhamisi) na kusisitiza kuwa, watu wa aina hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria. Tume hiyo pia imesisitiza kuwa uchaguzi wa leo nchini Uganda utakuwa huru na wa haki.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Badru Kiggundu amesema, kuna njama za kuchapishwa makaratasi yanayofanana na yale ya kupigia kura na ambayo tayari yametiwa alama ili kuipotezea itibari tume yake na kuchochea umma kwamba kumefanyika udanganyifu.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Uganda ametoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria za uchaguzi ambao umeanza muda mfupi uliopita. Mhandisi Badru Kiggundu amesema pia kuwa, hii ndio mara yake ya mwisho kusimamia uchaguzi nchini Uganda. Muhula wa pili na wa mwisho wa mhandisi huyo unamalizika mwezi Novemba mwaka huu.

Tayari vituo vya kupigia kura vimefunguliwa na zoezi la kuwachagua viongozi wapya limeanza. Nafasi ya Urais imewavutia wagombea 8 akiwemo Rais Yoweri Museveni na Waziri Mkuu wa zamani, Amama Mbabazi pamoja na mpinzani wa muda mrefu wa serikali, Dk. Kizza Besigye.

Tags