Matatizo ya wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1498-matatizo_ya_wakimbizi_wa_burundi_nchini_tanzania
Karibu wakimbizi 130,000 kutoka Burundi wameingia Tanzania kufuatia mgogoro unaoendelea ndani ya nchi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2016 21:57 UTC
  • Matatizo ya wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania

Karibu wakimbizi 130,000 kutoka Burundi wameingia Tanzania kufuatia mgogoro unaoendelea ndani ya nchi yao.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania imesema tokea uanze mgogoro wa kisiasa nchini Burundi mwezi Aprili mwaka 2015 hadi sasa, takribani wakimbizi 129,210 wameingia Tanzania.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, Issac Nantanga ameongeza kuwa wakimbizi Warundi wangali wanaendelea kumiminika Tanzania. Katika idadi hiyo, wakimbizi 79,290 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu na wengine 45,487 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo na 4,543 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi Mtendeli iliyopo wilayani Kakonko mkoani Kigoma.

Takribani watu laki mbili wamekimbia Burundi tokea mwezi Aprili mwaka jana kufuatia mgogoro ulioibuka nchini humo baada ya Rais Pierre Nkrunziza kutangaza nia yake ya kuwania urais kwa muhula wa tatu mfululizo. Nkurunziza alishinda uchaguzi huo wa mwezi Julai mwaka jana na hadi wakati huu nchi hiyo, hasa mji mkuu, Bujumbura, imekuwa ukisumbuliwa na machafuko na mauaji ya mara kwa mara. Hali hiyo imewalazimisha raia wa nchi hiyo waendelee kukimbilia nchi jirani hasa Tanzania.

Hivi sasa kuna wasiwasi kuwa wakimbizi Warundi wataanza kufukuzwa nchi walizokimbilia. Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo alisema kuwa nchi yake inaweza kuwafukuza makumi ya wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo na kuwapeleka nchi nyingine. Alitoa kauli hiyo baada ya serikali ya Burundi kuituhumu Rwanda kuwa inatoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi Warundi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Baadhi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni walisema serikali ya Rwanda inatekeleza njama za kuvuruga usalama nchini Burundi.

Wakuu wa Rwanda wamepinga vikali tuhuma hizo. Wakuu wa Rwanda wamekutana na mwakilishi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na kumhakikishia kuwa wakimbizi Warundi hawatafukuzwa.

Rais Nkurunziza wa Burundi hivi karibuni alipinga vikali pendekezo la Umoja wa Afrika kutuma askari 5,000 wa kulinda amani ncini humo. Alitishia kuwa iwapo walinda amani hao Waafrika wataingia nchini humo bila idhini ya serikali ya Burundi, basi watahesabiwa kama wavamizi na jeshi la nchi hiyo litapambana nao.

Kufuatia vitisho hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika limebatilisha uamuzi wa kutuma askari Burundi. Duru zinadokeza kuwa viongozi watano wa nchi za Kiafrika wakiwakilisha Umoja wa Afrika wanatazamiwa kwenda Burundi hivi karibuni kujaribu kutatua mgogoro wa nchi hiyo.

Nchi za Kiafrika zingali zinafuatilia kwa karibu jitihada za kusuluhisha mgogoro wa Burundi. Hivi karibuni Ismail Chanti, mkuu wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASAF) alisema kikosi hicho kiko tayari kujiunga na vikosi vingine vya Afrika kulinda amani nchini Burundi iwapo serikali ya nchi hiyo itaafiki.