Maelfu ya waasi waweka chini silaha nchini Sudan
Maelfu ya waasi wa harakati ya SPLM tawi la Abdul Wahid Nour wameweka chini silaha zao nchini Sudan.
Ripoti zinasema kuwa zaidi ya waasi elfu tatu wanachama wa kundi la SPLM tawi la Abdul Wahid Muhammad Nour wamekabidhi silaha zao. Waasi hao walikuwa wakipigana na jeshi la serikali ya Sudan huko kaskanizi na magharibi mwa eneo la milimani la Jabal Murrah katika jimbo la Darfur. Baada ya kukabidhi silaha, waasi hao wameingia makao makuu ya Darfur ili kuanza mazungumzo na serikali ya Khartoum.
Mkuu wa kundi hilo la waasi, Yusuf Is'haq amesema wapiganaji 3,660 wa kundi la SPLM wamekabidhi silaha zao baada ya kupigana na serikali ya Sudan kwa kipindi cha miaka 15 baada ya kutambua kwamba vita havina faida. Amesema kundi hilo limeanza mazungumzo na serikali ya Sudan na kwamba zinafanyika jitihada za kuwashawishi waasi wengine ili waweke chini silaha zao na kujiunga na mwenendo wa mapatano.