Waislamu wa Nigeria wahofia usalama wa Sheikh Zakzaky
Harun al-Binawi mjumbe wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, amefafanua mazingira na hali mbaya anayoipitia Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi mkuu wa harakati hiyo.
Al-Binawi ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Tasnim na kusisitiza kuwa, kitendo cha kumtia mbaroni Sheikh Zakzaky na mkewe kilichojiri katika tukio la hujuma ya kutisha ya askari wa nchi hiyo na kisha kuendelea kuwashikilia shakhsia hao katika mazingira magumu, ni uvunjaji wa wazi wa haki za binaadamu. Mwanaharakati huo wa Kiislamu nchini Nigeria ameongeza kuwa, katika hujuma hiyo ya kikatili, askari walimpiga risasi sita sheikh Zakzaky, huku wakimpiga mke wake risasi mbili. Aidha Sheikh Harun al-Binawi amesema kuwa, katika mazingira hayo, serikali ya Nigeria, imekuwa ikiwazuia mawakili na watu wa karibu, kumuona kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu nchini humo. Al-Binawi, aliyekuwepo wakati wa kujiri hujuma hiyo ya jeshi la Nigeria hapo tarehe 12 na 13 mwezi Disemba mwaka jana, ambapo karibu watu 1000 waliuawa, amesema kuwa jinai hiyo dhidi ya Waislamu ilijiri baada ya kuratibiwa na idara maalumu. Amesisitiza kuwa, askari hao wasiokuwa na utu wala ubinaadamu, walikuwa wakiwamiminia risasi Waislamu waliokuwa tayari wamejeruhiwa, huku wakiwachoma na ncha za silaha zao wanawake waliokuwepo eneo la tukio na pia kuwadhalilisha, suala ambalo liliyafanya mandhari kuwa ya kutisha zaidi. Al-Binawi amesema kuwa, kile kilichotokea Zaria, ni jinai za wazi za kivita na kwamba hivi sasa Waislamu wa Nigeria wanataka kuona wahusika wa jinai hizo wakichukuliwa hatua za kisheria.