Umoja wa Mataifa: Tanzania ni ya kupigiwa mfano "elimu kwa wote"
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema kuwa, utashi wa kisiasa, matumizi ya Pato la Taifa na matumizi ya fursa mbalimbali unaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi ya kupigiwa mfano katika uboreshaji na upatikanaji wa elimu kwa wote.
Ban Ki-moon amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Kamisheni ya Kimataifa kuhusu, “Kizazi kinachojifunza: Uwekezaji katika elimu kwa dunia inayobadilika” iliyofanyika katika Makao Makuu ya UN na kuhudhuriwa karibu na makamishna wote wanaounda tume hiyo akiwamo Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Tume hiyo ambayo ipo chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Katika Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, David Cameroon inawahusisha pia baadhi ya marais waliopo madakarani, mawaziri wakuu waliopo madarakani na waliostaafu.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), wawekezaji wakubwa akiwamo tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote, taasisi za utafiti, wataalamu wa masuala ya fedha, asasi za kijamii na makundi ya vijana wakiwamo wanafunzi.
“Uzoefu wa nchi kama Tanzania, Vietnam na nchi yangu mwenyewe Korea, unaonesha kwamba pale ambapo pana utashi wa kisiasa, ukijumuishwa na uwepo wa fursa na raslimali fedha kuna kitu kinachoweza kufanyika katika elimu,” alisema Ki-moon.
Na kutokana na uzoefu wa nchi kama Tanzania na nyinginezo, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Jumuiya ya Kimataifa ni lazima iwe tayari kuzisaidia kwa mitaji nchi ambazo zimeamua na kujituma katika kuifanyia mageuzi mifumo yake ya elimu na kujipati matokeo yanayoridhisha.