Tume: Yumkini uchaguzi mkuu usifanyike mwezi ujao DRC
(last modified Sun, 02 Oct 2016 08:16:17 GMT )
Oct 02, 2016 08:16 UTC
  • Tume: Yumkini uchaguzi mkuu usifanyike mwezi ujao DRC

Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema huenda uchaguzi mkuu usifanyike nchini humo mwezi ujao wa Novemba kama ilivyotarajiwa kutokana na sababu za kilojistiki.

Mkuu wa tume hiyo Corneille Nangaa amewaambia wajumbe wa vyama vya kisiasa kuwa, tume hiyo ipo mbioni kutathmini daftari la wapiga kura na kwamba zoezi hilo linatazamiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka ujao 2017. Aidha amesema tume hiyo itahitaji siku 504 zaidi ili kuandaa uchaguzi wa rais na kwamba wakati mwafaka wa kufanyika uchaguzi huo ni Disemba mwaka 2018.

Tayari Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekanusha madai kuwa yeye ndiye aliyesababisha kuahirishwa kwa uchaguzi huo na kusisitiza kuwa ucheleweshaji huo umetokana na sababu za kilojistiki.

Rais Joseph Kabila wa Congo DR

Rais Kabila mwenye umri wa miaka 45 ambaye yupo madarakani tangu kuuliwa baba yake mwaka 2001, anakabiliwa na mashinikizo ya ndani na ya madola makubwa yanayomtaka aachie madaraka na kuitisha uchaguzi wa rais baada ya muhula wake kumalizika mwezi ujao wa Novemba.

Hii ni katika hali ambayo, vyama vikuu vya upinzani vimesusia mazungumzo ya kitaifa yaliyoanza Ijumaa iliyopita jijini Kinshasa, chini ya upatanishi wa Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo.

Tags