Waziri wa Kigeni Kenya, Amina Mohammad, kuwania uenyekiti wa Tume ya AU
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16606-waziri_wa_kigeni_kenya_amina_mohammad_kuwania_uenyekiti_wa_tume_ya_au
Serikali ya Kenya imewasilisha jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bi. Amina Mohamed kuwa mwenyekiti ajaye wa Tume ya Umoja wa Afrika AU.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 03, 2016 11:36 UTC
  • Waziri wa Kigeni Kenya, Amina Mohammad, kuwania uenyekiti wa Tume ya AU

Serikali ya Kenya imewasilisha jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bi. Amina Mohamed kuwa mwenyekiti ajaye wa Tume ya Umoja wa Afrika AU.

Bi. Mohamed atachuana na Agapito Mba Mokuy wa Equatorial Guinea, Abdoulaye Bathily wa Senegal na Pelonomi Venson-Moitoi wa Botswana ambao nao wanataka uenyekiti huo.

Akitoa taarifa kuhusu Kenya kumpendekeza Bi. Mohamed kuwania wadhifa huo, Rais Uhuru Kenyatta amesema, "Naona Amina amekuwa na utendaji kazi mzuri na hivyo tumempendekeza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya AU,"

Uchaguzi wa wanachama wa Tume ya AU ulikuwa ufanyike Kigali, Rwanda, Julai 2016 wakati wa mkutnao wa kilele wa viongozi wa Afrika lakini baada ya duru saba za upigaji kura, hakuna yeyote kati ya wagombea watatu aliyepata thuluthi tatu za kura zinazohitajika kushinda.

Nkosozana Dlamini-Zuma

Kiti hicho kiko wazi baada ya kumalizika muda wa mwenyekiti wa sasa, Bi. Nkosazana Dlamini-Zuma wa Afrika kusini ambaye aliteuliwa mwaka 2012 lakini hakuwania tena muhula wa pili. Uchaguzi huo unatazamiwa kufanyika Januari 2017. Bi. Mohamed amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na pia naibu mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP mbali na kushikilia nyadhifa mbali mbali katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya.