Wahajiri 5,600 wanusurika kifo katika pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16651-wahajiri_5_600_wanusurika_kifo_katika_pwani_ya_libya
Gadi ya ulinzi wa pwani ya Italia imesema wahajiri wapatao 5,600 wamenusurika kifo katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterranean wakielekea bara Ulaya jana Jumatatu; idadi inayotajwa kuwa kubwa zaidi ya wahajiri kuokolewa katika siku moja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2016 04:25 UTC
  • Wahajiri 5,600 wanusurika kifo katika pwani ya Libya

Gadi ya ulinzi wa pwani ya Italia imesema wahajiri wapatao 5,600 wamenusurika kifo katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterranean wakielekea bara Ulaya jana Jumatatu; idadi inayotajwa kuwa kubwa zaidi ya wahajiri kuokolewa katika siku moja.

Mmoja wa maafisa wa gadi hiyo amewaambia waandishi wa habari kuwa, wahajiri zaidi ya 700 wameokolewa wakiwa ndani ya boti moja ya mpira katika moja ya operesheni 20 za uokoaji zilizofanyika jana karibu na kisiwa cha Lampedusa, katika pwani ya Italia.

Habari zaidi zinasema kuwa miili tisini imeweza kupatikana katika shughuli za uoakoaji, umbali wa kilomita 30 kutoka pwani ya Libya.

Wahajiri wa Kiafrika wakielekea bara Ulaya

Septemba 14, Maafisa wa gadi ya kulinda fukwe za Italia walitangaza habari za kuwaokoa wahajiri 650 waliokuwa wamejazana kwenye boti sita zilizokuwa zimepakia watu kupindukia na ambazo zilikuwa zikirushwa na mawimbi huko na huko katika fukwe za Libya, katika operesheni iliyofanyika kwenye bahari ya Mediterranean.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na  Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM zinaonesha kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 hadi sasa, karibu wahajiri laki moja na elfu 30 wameingia katika fukwe za Italia na wengi wao wametokea katika fukwe za Libya, huku zaidi ya 3,000 miongoni mwao wakiripotiwa kufa maji kabla ya kufika wanakokwenda, katika bahari ya Mediterranean.