Kutokubalika vitendo vya utumiaji mabavu vya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16669-kutokubalika_vitendo_vya_utumiaji_mabavu_vya_jeshi_la_nigeria_dhidi_ya_waislamu
Katika hali ambayo malalamiko dhidi ya kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky yangali yanashuhudiwa nchini Nigeria, jeshi la nchi hiyo limeongeza miamala yake ya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2016 08:28 UTC
  • Kutokubalika vitendo vya utumiaji mabavu vya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu

Katika hali ambayo malalamiko dhidi ya kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky yangali yanashuhudiwa nchini Nigeria, jeshi la nchi hiyo limeongeza miamala yake ya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu.

Jumatatu ya jana msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alitangaza kuwa, vitendo vya jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu havikubaliki hata kidogo. Akizungumza mjini Kaduna Ibrahim Mussa amepinga madai ya uchochezi dhidi ya harakati hiyo na kusisitiza kwamba, katika kipindi chote cha miongo kadhaa ya harakati za kijamii na kisiasa Harakati ya Kiislamu ya Mashia nchini Nigeria hakuna wakati ambao ilijihusisha na vitendo visivyo halali na vya utumiaji mabavu.

Katika sehemu nyingine ya taarifa yake, Ibrahim Mussa amesisitiza juu ya udharura wa kukomeshwa vitendo vya utumiaji mabavu vya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu na kumuachilia huru haraka Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa harakati hiyo. Pamoja na kuwa, kwa miaka nenda rudi Waislamu wa Nigeria wakiwemo Masuni na Mashia na wafuasi wa dini nyingine wamekuwa wakiishi kwa amani, utulivu na kuheshimiana baina yao, lakini mwaka uliopita jeshi la Nigeria lilivamia makazi ya Sheikh Zakzaky Kiongozi wa Mashia nchini humo na kutia dosari utulivu wa kisiasa uliokuwa ukitawala katika nchi hiyo.

Disemba mwaka jana, jeshi la Nigeria lilivamia Husseiniyah ya Baqiyatullah mjini Zaria na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia na kumjeruhi vibaya Sheikh Zakzaky na kisha kumtia rumande.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Jeshi la Nigeria lilidai kuwa, wafuasi wa Sheikh Zakzaky walitaka kumuua Mkuu wa majeshi ya Nigeria, madai ambayo yanapingwa vikali na Waislamu hao. Katika hali ambayo umepita karibu mwaka mmoja tangu Sheikh Zakzaky atiwe mbaroni huku kukiwa na taarifa za kuzorota afya ya mwanazuoni huyo wa Kiislamu, juhudi zote za kutaka kuachiliwa kwake huru mwanazuoni huyo zimegonga ukuta. 

Miji kadhaa ya Nigeria imekuwa ikishuhudia kushadidi maandamano yanayotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky. Kuongezeka maandamano hayo kunakwenda sambamba na kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu vya vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji hao, kiasi kwamba, wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, chuki na hasama za jeshi la Nigeria dhidi ya jamii kubwa ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, jambo ambalo limezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali hususan Waislamu wa Kishia.

Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, lengo la jeshi la Nigeria la kumtia mbaroni Sheikh Ibrahim Zakzaky ni kuisambaratisha Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Wafuasi wa madhehebu ya Kishia nchini Nigeria wanaamini kuwa, kuna vibaraka katika jeshi la Nigeria ambao kwa muda wamekuwa wakichochewa na baadhi ya madola ya kigeni ili wawashinikize Waislamu hao.

Sheikh Ibrahim Zakzaky alipoteswa na jeshi la Nigeria 

Baadhi ya wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni una mkono katika matukio ya kukandamizwa Waislamu wa Kishia nchini Nigeria. Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi nazo zinatajwa kuhusika na njama za kuzusha hitilafu baina ya Waislamu na kupanua satwa yao katika eneo hilo la Afrika.

Masuala hayo yanatajwa kuwa ndiyo yanayoandaa mazingira ya kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky bila ya sababu yoyote na hivyo kuendelea kuitesa jamii ya Kiislamu nchini Nigeria. 

Walimwengu wanataraji kuiona serikali ya Nigeria ikichukua hatua za kushughulikia suala hilo hasa kutokana na ombi la Waislamu na hivyo kufungua mlango wa kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.