Wananchi wa Niger washiriki uchaguzi wa rais
Wananchi wa Niger waliotimiza masharti ya kupiga kura, leo wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kumchagua rais atakayeiongoza nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, ambayo kwa muda sasa imekuwa ikikabiliwa na shambulio moja baada ya jingine kutoka kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi leo kwa saa za nchi hiyo huku idadi ndogo ya wapiga kura ikijitokeza kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Niger uchaguzi wa Bunge umefanyika sambamba na ule wa rais. Miongoni mwa wagombea wa kiti cha rais ni Rais wa hivi sasa Mahamadou Issoufou anayewania kuongoza kwa muhula wa pili na mpinzani wake wa karibu Hama Amadou.
Amadou aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Niger kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya magendo ya watoto. Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa amekimbilia Ufaransa, alirejea nchini humo Novemba 14 mwaka uliopita. Mara tu baada ya kurejea vyombo vya usalama vilimtia mbaroni. Pamoja na kuendelea kushikiliwa korokoroni, Mahakama ya Katiba ilimuidhinisha kuwa miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais. Hama Amadou anaamini kwamba, kutiwa kwake mbaroni kuna sababu za kisiasa. Mwingine anayetazamiwa kutoa ushindani mkali kwa Rais Issoufou, ni Seyni Oumaru, mkuu wa muungano wa upinzani nchini humo. Iwapo hakuna mgombea wa urais atakayepata ushindi wa zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, uchaguzi huo wa rais utaingia duru ya pili.
Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini muhimu ya urani, Niger inahesabiwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani.