Wanajeshi wa Russia wawasili Misri kwa ajili ya manuva ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17404-wanajeshi_wa_russia_wawasili_misri_kwa_ajili_ya_manuva_ya_kijeshi
Kundi moja la wanajeshi maalumu wa kikosi cha anga wa Russia wamewasili Misri kwa lengo la kushiriki kwenye manuva ya kijeshi dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2016 10:55 UTC
  • Wanajeshi wa Russia wawasili Misri kwa ajili ya manuva ya kijeshi

Kundi moja la wanajeshi maalumu wa kikosi cha anga wa Russia wamewasili Misri kwa lengo la kushiriki kwenye manuva ya kijeshi dhidi ya ugaidi.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imeripoti kuwa, wakiwa nchini MIsri, wanajeshi hao watafanya mazoezi katika eneo la jangwani. Luteka hiyo imepewa jina la "Mazoezi ya Ulinzi ya Kirafiki mwaka 2016"  na wanajeshi wa Russia watakuwa pamoja na wanajeshi wa Misri katika oparesheni ya kimajaribio ya kuyaangamiza makundi ya kigaidi na yale yenye silaha.

Ripoti ya Wizara ya Ulinzi ya Russia imeongeza kuwa, oparesheni kuu zaidi ya wanajeshi hao wa kikosi maalumu cha anga cha nchi hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika huko Misri, itafanyika kwa kutumia helikopta na miavuli ili kupambana na magaidi katika mazingira magumu ya jangwani kwa kushirikiana na wanajeshi wa Misri.

Wanajeshi wa anga wa Russia wakijiandaa kwa manuva yao huko Misri

Hii ni katika hali ambayo idadi ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Russia wanaoshiriki kwenye manuva hiyo ya kijeshi huko Misri haijafahamika na imeelezwa kuwa upo uwezekano Misri ikaandaa utaratibu wa kupewa mafunzo wanajeshi wao katika maneva hayo. Wiki iliyopita Russia ilitangaza habari ya kutaka kutuma wanajeshi wake katika kambi yake ya kijeshi ya zama za Umoja wa Kisovieti iliyoko Sidi Barran nchini Misri.