Meli za kivita za Iran zazima hujuma ya maharamia karibu na Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17641-meli_za_kivita_za_iran_zazima_hujuma_ya_maharamia_karibu_na_somalia
Meli za kivita za Iran zimefanikiwa kuzima hujuma kadhaa za maharamia waliolenga kuziteka meli mbili za kibiashara za Iran katika Ghuba ya Aden.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2016 23:41 UTC
  • Meli za kivita za Iran zazima hujuma ya maharamia karibu na Somalia

Meli za kivita za Iran zimefanikiwa kuzima hujuma kadhaa za maharamia waliolenga kuziteka meli mbili za kibiashara za Iran katika Ghuba ya Aden.

Msafara wa 44 wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, unaojumuisha manowari za Alvand na Bushehr, ulinusuru meli mbili za kibiashara za Iran ambazo zilishambuliwa mara tatu na maharamia Jumatatu asubuhi.

Maharamia hao, ambao hutoka katika pwani ya Somalia, walishambulia meli ya kwanza ya mizigo ya Iran wakitaka kuiteka nyara lakini walilazimika kutoroka baada ya kufyatuliwa  risasi na manowari za Iran.

Baada ya hapo maharamia hao walijaribu tena kuiteka nyara meli ya kibiashara ya Iran wakiwa wamejizatiti na boti nane za kasi na wakafanya tena jaribio la pili wakiwa na boti 13 zilizokuwa na silaha nzito nzito. Hujuma hizo zote mbili zilizuiwa kwa mafanikio na manowari za kivita za Iran na hivyo maharamia wakalazimika kulitoroka eneo hilo.

Manoari ya kivita ya Iran

Msafara huo wa 44 wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliekelea katika maji ya kimataifa Oktoba 5 kulinda  njia za baharini zinazotumiwa na meli za kibiashara.

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran Admeli Habibollah Sayyari alisema mwezi Septemba kuwa, majeshi ya wanamaji Iran wamesindikiza meli za kibiashara na mafuta zaidi ya 3,200 za Iran na  zisizo za Iran katika kipindi cha miezi sita. Jeshi la Wanamaji la Iran limefanikiwa kuzuia hujuma nyingi za maharamia dhidi ya meli za Iran na za kigeni katika maji ya kimataifa.