Ugaidi Mashariki ya Kati, Afrika umezushwa na nchi za Magharibi
Nchi za Magharibi ndizo zilizozusha na kueneza ugaidi barani Afrika na eneo zima la Mashariki ya Kati.
Hayo yamesemwa na Ivan Ippolitov mtaalamu wa Taasisi ya Masomo ya Kistratijia nchini Russia katika mahojiano na Shirika la Habari la Iran, IRNA ambapo ameashiria matukio ya hivi karibuni Mashariki ya Kati na nafasi ya Marekani katika kuzuka migogoro ya eneo hili.
Amesema Marekani imekuwa ikizusha migogoro na misuguano baina ya nchi mbali mbali duniani na kwamba jambo hili linaonekana wazi Mashariki ya Kati. Mtaalamu huyo wa Russia amesema moja ya sera za Marekani ni kuzusha migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati au Magharibi mwa Asia.
Ivan Ippolitov ameongeza kuwa, Marekani imechukua hatua hizo dhidi ya nchi ambazo haziafikiani na sera zake ili kuzidhoofisha.
Mtaalamu huyo wa Russia amesema Marekani imekua ikifuatilia sera za kulea na kuzusha magaidi katika eneo la Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati na kuwa jambo hilo limezusha matatizo makubwa. Amesema njia pekee ya kumaliza mgogoro uliopo ni nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya mataifa ya eneo.