Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia ataka kukomeshwa machafuko ya kisiasa kote nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18538-waziri_wa_ulinzi_wa_ethiopia_ataka_kukomeshwa_machafuko_ya_kisiasa_kote_nchini
Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia amesisitiza juu ya kukomeshwa haraka iwezekanvyo machafuko ya kisiasa katika maeneo yote ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2016 23:06 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia ataka kukomeshwa machafuko ya kisiasa kote nchini

Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia amesisitiza juu ya kukomeshwa haraka iwezekanvyo machafuko ya kisiasa katika maeneo yote ya nchi hiyo.

Siraj Fegessa ameyataka makundi yote ya kisiasa nchini Ethiopia kuhitimisha maandamano ya utumiaji mabavu ya kisiasa katika nchi hiyo na kutoruhusu anga ya kisiasa ya nchi hiyo kukumbwa na vurugu na ukosefu wa amani.

Waziri wa vikosi vya ulinzi wa Ethiopia ametangaza pia kuwa, hadi sasa raia elfu mbili waliokuwa wametiwa mbaroni nchini humo wakihusishwa na vurugu na machafuko ya hivi karibuni wameachiliwa huru na kwamba, wameachiwa huru kwa mujibu wa msamaha wa umma uliotangazwa na serikali. 

Maandamano ya kupinga serikali nchini Ethiopita

Maandamano na machafuko hayo ambayo yalianzia katika jimbo la Oromia katikati na magharibi mwa Ethiopia mwezi Novemba mwaka uliopita, yalienea na kufika katika jimbo la Amhara lililoko kaskazini mwa nchi. Ghasia hizo zilichochewa na uamuzi wa kiuchumi wa serikali wa kutaka kupanua eneo la mji mkuu Addis Ababa kwa kuwapokonya Waoromo mashamba yao ya kilimo.

Maandamano makubwa ambayo yamekuwa yakifanywa na makabila hayo mawili ya Oromo na Amhara ambayo yanaunda karibu asilimia 60 ya watu wote wa nchi hiyo yamevuruga utulivu wa kijamii na kisiasa katika nchi hiyo ya eneo la Pembe ya Afrika.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanavituhumu vyombo vya usalama kwamba, vimekuwa vikiyakandamiza maandamano ya raia hao kwa mkono wa chuma.