Uhuru: Kenya haijutii kuwaondoa wanajeshi wake Sudan Kusini
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema taifa hilo halijuti kwa uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki walioko Sudan Kusini chini ya mwavuli wa kikosi maalumu cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa (UNMISS).
Akiongea katika hafla ya kufuzu makurutu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF katika Chuo cha Kijeshi cha Lanet katika kaunti ya Nakuru, Rais Kenyatta amesema usalama wa kieneo haufai kupatikana kwa kudhalilishwa, kukejeliwa na kushushwa hadhi na fahari taifa la Kenya. Rais wa Kenya amebainisha kuwa, nchi hiyo itajiondoa kikamilifu katika mchakato wa kuupatia ufumbuzi mzozo wa Sudan Kusini.
Hapo jana, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya ilitangaza kuwa itawaondoa wanajeshi wake walioko Sudan Kusini baada ya kamanda wake kutimuliwa kazini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimfuta kazi Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki baada ya ripoti ya uchunguzi kusema alikosa kuwajibika kulinda raia mapigano yalipozuka upya nchini Sudan Kusini mwezi Julai mwaka huu. Ripoti hiyo ilisema, walinda amani waliokuwa chini ya jenerali huyo wa Kenya hawakuchukua hatua yoyote ya kuwalinda raia wakati wanajeshi wa serikali waliposhambulia kituo cha utoaji misaada mjini Juba.
Hii ni katika hali ambayo, polisi nchini Kenya inamshikilia katika kituo cha uwanja wa ndege wa JKIA jijini Nairobi, James Gatdet Dak, msemaji wa Riek Machar, kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini huku duru za habari zikiripoti kuwa, huenda akarejeshwa katika nchi yake au nchi ya tatu itakayokubali kumpokea.