Jamhuri ya Kongo nayo inajiandaa kujiondoa ICC?
Wimbi la nchi za Afrika kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC limeendelea kushuhudiwa barani humo huku vyama vya siasa katika Jamhuri ya Kongo Brazaville vikiitaka serikali ya nchi hiyo ifuate mkondo huo.
Vyama viwili vikuu ndani ya muungano tawala nchini humo vya Patriotic Front na 2020 Awakening Movement, vimemkabidhi Waziri wa Sheria Pierre Mabiala, waraka wenye kufafanua sababu za vyama hivyo kuitaka nchi hiyo ijiondoe ICC.
Waziri huyo amesema anadurusu hoja zilizotolewa na vyama hivyo kabla ya kuwasilisha rasmi pendekezo hilo kwa serikali. Vyama hivyo vinasema sheria zinazoendesha mahakama hiyo ya mjini The Hague haziendani na katiba ya nchi hiyo ya Kiafrika, haswa suala la kukabidhi raia wake kwa nchi au taasisi nyingine.
Nchi za Afrika Kusini, Burundi na Gambia tayari zimeanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi.
Nchi zingine kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.
Hata hivyo, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC siku chache zilizopita alisema licha ya kuwa mahakama hiyo imepata pigo kufuatia hatua ya nchi tatu za Afrika kuanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma, lakini hatua hiyo haiwezi kuzuia wala kutatiza shughuli za kila siku za mahakama hiyo.