Al-Sisi akiri ndege ya Russia ilitunguliwa na magaidi Misri
Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri amekiri kwamba ndege ya abiria ya Russia iliyoanguka mwezi oktoba mwaka uliopita katika anga ya nchi yake ilitunguliwa na magaidi.
Al-Sisi amesema magaidi waliotungua ndege ya shirika la Kogalymavia la Russia katika eneo la Sharm el-Sheikh, walikuwa na lengo la kulemaza sekta ya utalii ya Misri sambamba na kuvuruga uhusiano wa Cairo na Moscow.
Rais wa Misri amekuwa akikanusha madai ya kundi la kigaidi la Daesh kuwa lilitungua ndege hiyo mwezi Oktoba mwaka uliopita. Al-Sisi amekuwa akisema magaidi hawana uwezo wa kutekeleza hujuma kama hiyo kutokana na ulinzi mkali wa anga na nchi kavu kutoka kwa vyombo vya usalama vya Misri.
Tukio hilo la kuangushwa ndege ya abiria lilisababisha watu Sharm 224 kupoteza maisha; wengi wakiwa ni watalii kutoka nchini Russia. Vyombo vya usalama vya Russia vilibaini kwenye uchunguzi kwamba ndege hiyo ilianguka baada ya kupigwa bomu.