AU yasema mzozo wa Libya hauhitaji suluhisho la kijeshi
Viongozi wa Umoja wa Afrika AU wanakutana nchini Ethiopia kujadili mgogoro wa kisiasa na kiusalama unaoikabili Libya kwa sasa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia hapo jana, Rais Idris Deby wa Chad alisema jamii ya kimataifa inafaa kufahamu fika kuwa, kutumwa vikosi vya jeshi kutatua mgogoro wa Libya hakutakuwa na natija yoyote ghairi ya kuvuruga zaidi mambo. Ameongeza kuwa, kizingiti kikuu katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Libya ni misimamo mikali inayoshikiliwa na kambi mbili za kisiasa nchini humo na kwamba hilo linahitaji mazungumzo na sio suluhu ya kijeshi.
Kwa upande wake, Nkosazana Dlamini-Zuma, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amezitaka serikali za nchi za bara hilo kuongeza misaada ya kibinadamu kwa maeneo yaliyoathirika na mzozo huo. Amesema Walibya milioni 2.4 wakiwemo wakimbizi wa ndani laki 3 na elfu 50 wanahitaji misaada ya dharura ya kibinadamu.
Marais na viongozi wa serikali kutoka nchi za Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Niger, Afrika Kusini, Sudan na Uganda wanahudhuria mkutano huo ulioanza hapo jana.
Tunisia itakuwa mwenyeji wa kikao cha kimataifa cha kujadili mgogoro wa Libya mapema mwakani. Nchi 5 za kaskazini mwa Afrika na 5 za kusini magharibi mwa eneo la Mediterania zimekubali pendekezo la Tunisia la kuwa mwenyeji wa kikao hicho cha kimataifa kilichopangwa kufanyika mapema mwakani ili kuchunguza hali ya mambo ya Libya.
Mgogoro wa kisiasa nchini Libya ulianza baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 na mbali na mgogoro huo, nchi hiyo inashuhudia harakati za kundi la kigaidi la Daesh.